VIONGOZI WAJITOSA KUKOMESHA UTUMIKISHWAJI WA WATOTO




Na Carlos Claudio, Dodoma.


Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, amewataka waajiri wote nchini kuhakikisha hawahusiki kwa namna yoyote na vitendo vya utumikishwaji wa watoto katika maeneo ya kazi, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kukiuka agizo hilo.


Mhe. Katambi ametoa kauli hiyo leo, Juni 12, 2025, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto, ambayo huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 12 Juni.


Amesema kuwa serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na vitendo vya utumikishwaji wa watoto, hali iliyopelekea kupungua kwa matukio hayo kutoka asilimia 29 mwaka 2014 hadi asilimia 24.9 mwaka 2025, kwa mujibu wa utafiti wa Nguvu Kazi wa mwaka 2021.


“Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Tumeidhinisha mikataba mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Mkataba wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 unaolinda na kutetea haki za watoto,” amesema Mhe. Katambi.


Aidha, amebainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni matokeo ya ushirikiano baina ya serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Hata hivyo, amesisitiza  kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayehusishwa katika kazi zinazowanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu, afya bora na mazingira salama ya makuzi.


“Siku hii ya kimataifa inatukumbusha wajibu wetu wa pamoja kama taifa na kama jamii kuhakikisha watoto wote wanalelewa katika mazingira salama na yenye heshima kwa utu wao. 


Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaoendeleza vitendo hivi viovu,” aliongeza.


Maadhimisho haya yameambatana na kauli mbiu inayosisitiza wajibu wa pamoja katika kuwalinda watoto dhidi ya ajira hatarishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa kutokomeza kabisa utumikishwaji wa watoto ifikapo mwaka 2025.


Kwa upande wake, Mratibu wa miradi kitaifa kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Glory Blasio Emmanuel, amesema kuwa zaidi ya watoto milioni 160 duniani wanatumikishwa, huku wengi wakijihusisha na kazi hatarishi, hasa katika kilimo.


“Mtoto wa kike bado anaathirika zaidi, hasa katika ajira za ndani ambazo mara nyingi hufanyika kwa siri na bila ulinzi wa kisheria,” alisema Glory Blasio. 


Ameongeza kuwa asilimia 24.9 ya watoto hao wanahusika na kazi mbaya zaidi kama migodini, usafirishaji haramu na unyanyasaji wa aina mbalimbali.


Glory Blasio ametoa wito kwa nchi wanachama wa ILO kuwekeza zaidi kwenye ajira zenye staha kwa wazazi, kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za ajira kwa watoto ili kuondoa utegemezi wa kipato kutoka kwao.


Naye Kamishna wa Kazi, Susan K. Mkangwa, amesema Serikali kupitia Idara ya Kazi imeanza maandalizi ya kaguzi maalum katika mashamba, migodini na maeneo ya kazi ili kubaini watoto wanaotumikishwa na kuwachukulia hatua waajiri wote wanaohusika.


“Tutazindua kampeni za kitaifa za uelimishaji ili kuifikia jamii moja kwa moja. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mtoto anayepoteza haki yake ya elimu na utoto kwa sababu ya tamaa ya kipato cha haraka,” amesema Kamishna Mkangwa.









🚨Full VIDEO inapatikana kwenye Instagram Page yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post