TRA YATOA ONYO KALI KWA WANAOFANYA BIASHARA ZA MAGENDO.


Na Carlos  Claudio, Dodoma.


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejipanga kwa mkakati madhubuti wa kulinda viwanda vya ndani dhidi ya tishio la bidhaa haramu na magendo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2025/2026 ambayo imelenga kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuongeza mapato ya taifa.


Katika ziara ya ukaguzi wa viwanda jijini Dodoma, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema mamlaka hiyo imeunda kikosi maalum cha kudhibiti uingizwaji wa bidhaa kwa njia zisizo rasmi, hasa katika maeneo ya mipakani. 


Wafanyabiashara walionywa vikali dhidi ya tabia ya kughushi stika za kodi za kielektroniki maarufu kama Counterfeit Electronic Tax Tags, hatua aliyoitaja kuwa ni uhujumu uchumi na kosa kubwa kisheria.


“Tumejipanga kupambana na magendo, na tayari tumekamata bidhaa haramu nyingi zikiwemo Ethanol kutoka nje ya nchi. Wengi waliohusika walidai kodi ni kubwa, lakini Serikali sikivu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia na sasa kodi hizo zimepunguzwa,” amesema Kamishna Mwenda.


Katika ziara hiyo aliyoifanya kwenye viwanda vya Sun Land Agro na Meta kinachozalisha kinywaji cha Mwamba vilivyopo jijini Dodoma, Kamishna Mwenda ameeleza kuwa lengo kuu la serikali kupitia bajeti mpya ni kulinda viwanda vya ndani, hasa vinavyozalisha bidhaa za matumizi ya kila siku kama mafuta ya kula.


Moja ya njia tunazotumia kulinda viwanda hivi ni kwa kuvipa unafuu wa kodi. Serikali imesamehe kodi ya vyeti kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Vilevile, imeongeza kodi kwa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje na kudhibiti magendo katika bidhaa hizo, aliongeza.


Kamishna huyo alisisitiza kuwa uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa bora unazidi kuongezeka, akibainisha kuwa changamoto kubwa ni upatikanaji wa malighafi. Hata hivyo, ametoa wito kwa wakulima na wazalishaji wa ndani kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya viwanda hivyo.



TRA imeahidi kuwa bajeti hii mpya inalinda uzalishaji wa ndani na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa viwanda huku ikihakikisha bei za bidhaa hizo zinabaki kuwa nafuu kwa wananchi.


Tutahakikisha bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zinalindwa kwa kupunguziwa kodi na kufanya bidhaa hizo ziwe nafuu kwa Watanzania. Hii ndiyo roho ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayolenga kujenga uchumi wa viwanda kwa vitendo,” amesema Mwenda.


Mwisho, Kamishna Mwenda ametoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kufuata taratibu rasmi za forodha, kulipa kodi stahiki na kuepuka njia za mkato, akisema kuwa serikali itatumia nguvu zote za kisheria kulinda wale wanaozalisha kwa kufuata sheria na taratibu.












🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post