Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, leo amezindua rasmi jengo jipya la kupumzikia wananchi wanaowasubiri ndugu zao waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, akisisitiza kuwa huduma bora kwa wananchi ni kipaumbele chake.
Jengo hilo la kisasa, lililogharimu shilingi milioni 42, limejengwa kwa ushirikiano kati ya Mhe. Mavunde na wadau mbalimbali wa maendeleo, Tofauti na hali ya awali ambapo kulikuwa na kibanda kimoja kisicho na staha, jengo jipya limebuniwa kwa kuzingatia heshima na faragha ya jinsia, kwa kuligawanya sehemu ya wanawake na wanaume.
“Mimi kama Mbunge niliona ni wajibu wangu kushughulikia changamoto hii. Niliona wananchi wengi kutoka nje ya jiji la Dodoma wakilala au kukaa katika maeneo yasiyo rasmi, jambo ambalo halikubaliki kwa hadhi ya jiji hili. Ndiyo maana kwa kushirikiana na wadau tumejenga jengo hili jipya na la kisasa,” amesema Mhe. Mavunde.
Kaulimbiu ya uzinduzi huo ilikuwa “Huduma bora ni kipaumbele chetu – Karibu Tukuhudumie,” ikilenga kuonyesha dhamira ya kutoa huduma zenye ubora kwa jamii.
Wananchi waliopata nafasi ya kulishuhudia jengo hilo wamelipongeza juhudi za Mbunge huyo na kueleza kuwa hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya kusubiri wagonjwa katika mazingira magumu.
Uzinduzi huo ni sehemu ya mikakati ya kuboresha huduma katika sekta ya afya mkoani Dodoma, sambamba na kuwajali wananchi wanaoambatana na wagonjwa wao hospitalini.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.