Na Carlos Claudio, Dodoma.
Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika katika kijiji cha Mwitikira, kata ya Mwitikira jijini Dodoma, jumuiya na wadau wa maendeleo wameungana kuwatetea watoto na kuhimiza uwajibikaji wa jamii na serikali katika kulinda haki na ustawi wa mtoto wa Kitanzania.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Mawasiliano wa Shirika la Save the Children, Fedrick Shija, alitoa wito kwa serikali kuhakikisha huduma bora za afya na elimu kwa watoto zinaboreshwa, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa watoto wanaokumbwa na vitendo vya ukatili.
"Tunaiomba serikali iimarishe huduma za msingi kwa watoto – afya, elimu, pamoja na kuhakikisha mtoto anasikilizwa kulingana na mahitaji yake. Hii itasaidia watoto kufungua mioyo yao kueleza changamoto wanazopitia ambazo mara nyingi hufichika mbele ya jamii," alisema Shija.
Akaongeza kuwa njia bora ya kupambana na ukatili ni kwa watoto wenyewe kupewa nafasi ya kueleza wanayopitia, sambamba na kushirikishwa katika maamuzi ya familia na taifa. Alisisitiza kuwa kutoa sauti kwa watoto kutachangia katika kujenga
taifa lenye usawa na ustawi kwa vizazi vijavyo.
Shija pia alihamasisha familia kuanza kuhusisha watoto katika kupanga bajeti za familia, jambo ambalo litawajengea watoto misingi ya uwajibikaji na uelewa wa masuala ya maisha mapema kuanzia ngazi ya chini na taifa.
Kwa upande mwingine, Gift Emmanuel, mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Chiboli, aliwasilisha kilio cha wanafunzi wa vijijini kwa kuomba serikali kuongeza uwekezaji katika elimu kwa kujenga mabweni na kutoa vifaa vya kujifunzia.
"Tunaomba serikali kutujengea mabweni ili tusiendelee kutembea umbali mrefu kila siku kwenda shule. Pia vifaa vya kujifunzia ni changamoto kubwa kwa watoto wa vijijini. Tunahitaji msaada huu ili tuweze kufikia ndoto zetu," alisema Gift.
Watoto waliokuwepo kwenye maadhimisho hayo walikumbushwa kuhusu umuhimu wa kujiepusha na vitendo vinavyohatarisha maisha yao kama mimba za utotoni, ndoa za utotoni, na ajira hatarishi.
Wazazi na jamii kwa ujumla walihimizwa kuwapa watoto malezi bora, kuwa walinzi wa ndoto zao, na kuwasaidia kufikia malengo yao kwa kuwapa elimu na mazingira salama ya kukua.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 16 Juni, ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 waliokuwa wakidai haki yao ya kupata elimu bora.
Maadhimisho haya yanatoa fursa ya kutathmini mafanikio na changamoto katika kulinda haki za watoto barani Afrika.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Page yetu ya WASHINDI MEDIA.