NHIF YABORESHA HUDUMA KUPITIA MFUMO WA KIDIJITALI, YAWAHIMIZA WANANCHI KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA.


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, sambamba na kutangaza maboresho ya huduma zake kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali.


Akizungumza katika maonesho yanayofanyika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja wa NHIF, Bi. Angela Mziray, amesema kuwa NHIF imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.


“Sisi kama NHIF tupo hapa Chinangali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, ili mtu anapokumbwa na changamoto ya kuugua awe na uhakika wa kupata matibabu bila kikwazo cha gharama,” amesema Bi. Mziray.


Kwa sasa, wananchi hawalazimiki tena kufika ofisi za NHIF kwa ajili ya huduma mbalimbali. Kupitia mfumo wa NHIF Self Service, mwananchi anaweza kujisajili, kuongeza wategemezi, kupata taarifa za uanachama pamoja na matumizi ya bima kutumia simu au kompyuta binafsi.


“Wananchi wanaweza sasa kujisajili kupitia simu au laptop zao kwa kuingia kwenye tovuti ya NHIF (www.nhif.or.tz). Hata waajiri na vituo vya kutolea huduma wanaweza kujisajili moja kwa moja kupitia mfumo huu,” aliongeza.



Bi. Mziray ameweka wazi kuwa pamoja na usajili, mfumo huo pia unamwezesha mwananchi kutoa maoni, malalamiko au maswali kupitia sehemu maalum iliyopo kwenye tovuti ya NHIF, hatua inayolenga kuboresha zaidi huduma kwa mteja.


Aidha, ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanakuwa na bima ya afya, akisisitiza kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.


“Ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya. Serikali imeweka mazingira wezeshi, hivyo hatupaswi kusubiri hadi tuumwe ndipo tutafute fedha za matibabu,” alihitimisha.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post