KAMATI YA BAJETI YAIHAMASISHA SERIKALI KUBORESHA USAJILI WA MAJENGO KUKUSANYA KODI HALISI


Na Saida Issa, Dodoma.


KAMATI ya Bunge ya Bajeti imeishauri Serikali kukamilisha usajili wa majengo ili kodi ipangwe kwa kuzingatia thamani halisi ya nyumba, badala ya kiwango cha mfuto kinachotumika kwa sasa, hatua itakayoongeza mapato ya Serikali za Mitaa na kuziwezesha kujitegemea kimapato.


Mapendekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Manase Njeza, wakati akiwasilisha maoni kuhusu Tathmini ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/25, na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26, jijini Dodoma.


Njeza alisema licha ya kodi ya majengo kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa Serikali za Mitaa, bado haijachangia kikamilifu kutokana na changamoto ya usajili hafifu wa majengo. 


"kasi ya usajili ni ndogo kwa sababu ya ukosefu wa fedha, huku Halmashauri zikipokea asilimia 20 tu ya makusanyo ya kodi hiyo kwa ajili ya kazi ya usajili, kiwango ambacho hakitoshi, 


Katika kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Kamati imepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha mahusiano na Washirika wa Maendeleo, 


Taarifa inaonesha kuwa hadi Mei 2025, kiasi cha Shilingi trilioni 5.32 kilipokelewa kutoka kwa washirika hao, sawa na asilimia 87.5 ya lengo la mwaka, kutokana na usimamizi mzuri wa mikataba na matumizi ya fedha,"alisema. 


Aidha, Kamati ilieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilikusudia kukopa Shilingi trilioni 6.62 kutoka soko la ndani. 


Alisema kuwa Hadi Mei 2025, Shilingi trilioni 6.23 zilikuwa zimekopwa, sawa na asilimia 94.1 ya lengo hilo,Kamati imependekeza michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii iwekezwe zaidi kwenye dhamana za Serikali kutokana na usalama wake.


Kuhusu mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje, Kamati ilieleza kuwa Shilingi trilioni 2.43 zilipatikana hadi Mei 2025, sawa na asilimia 81.27 ya lengo la Shilingi trilioni 2.99. 


"Mafanikio hayo yalichangiwa na tathmini nzuri ya uwezo wa Tanzania kukopesheka, lakini Kamati imeshauri Serikali kupanua wigo wa vyanzo vya ndani kama hatifungani za manispaa na miundombinu, 


Katika matumizi ya bajeti, Kamati ilieleza kuwa hadi Mei 2025, Serikali ilikuwa imetoa ridhaa ya matumizi ya Shilingi trilioni 42.90, sawa na asilimia 85.31 ya bajeti yote,"alisema. 


Kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 30.63 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi trilioni 15.74 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post