POLISI DODOMA YATOA WITO WA AMANI NA USHIRIKIANO KUELEKEA SIKUKUU YA EID AL-ADHA.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuimarisha amani na kukabiliana na vitendo vya kihalifu vinavyoweza kuvuruga sherehe za Eid Al-Adha mwaka huu.


Akizungumza katika Msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi, amewaomba waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kusherehekea Eid kwa utulivu, upendo, na kufuata misingi ya dini pamoja na sheria za nchi.


“Tusherekee kwa amani na upendo, naomba msitoe mianya ya uhalifu kutokea, tuwe waangalifu na mali zetu, tusiachie watoto bila uangalizi na kila mmoja achukue tahadhari mapema,” amesema  Katabazi.


Kamanda huyo pia ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema endapo watabaini viashiria vya matukio ya kihalifu ili hatua stahiki zichukuliwe kabla ya madhara kutokea. 


Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limeimarisha doria katika maeneo yote ya Mkoa huo kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaendelea kudumishwa kipindi chote cha sikukuu.


Aidha, SACP Katabazi amesema kuwa Jeshi la Polisi halitarajii kusherehekea sikukuu ya amani kukumbwa na matukio ya uhalifu kama vile wizi, uvunjaji, ajali za barabarani au hata matukio mabaya kama mauaji ambayo huleta taharuki katika jamii.


Kwa kumalizia, Kamanda Katabazi amesisitiza kuwa mafanikio ya kudumisha amani ni jukumu la kila mmoja, hivyo ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi ni muhimu zaidi katika kufanikisha azma hiyo.








🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.





Previous Post Next Post