Na Hellen M. Minja,DODOMA RS.
Mkoa wa Dodoma upo kwenye Mpango Mkakati wa kukuza sekta ya Utalii kwa kujenga barabara na daraja kwenye mpaka wa Mkoa huo na Iringa uliopo katika Kijiji cha Ilangali Wilaya ya Chamwino litakalotumika kuunganisha wananchi wa Kata ya Manda na Hifadhi ya Taifa Ruaha ambapo itatengeneza fursa za kibiashara kwa Watalii watakaokwenda kwenye hifadhi hiyo kupitia Mkoani hapa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipofanya ziara ya kikazi kwenye eneo la mpaka lililopo kwenye Kijiji cha Ilangali, Kata ya Manda katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Juni 10, 2025.
"Tulianza kutengeneza Mpango Mkakati wa kukuza Utalii kwenye Mkoa wetu wa Dodoma ambapo kivutio kikubwa Mbuga ya Ruaha ambayo inapakana na Mkoa wetu wa Dodoma, ambapo tunajenga barabara na daraja la kutuvusha hapo ili tuweze kufika Ruaha na kuwe na njia ya kupita hapa kuingia 'Ruaha National Park".
Mhe. Senyamule ameongeza kuwa hiyo ni fursa ya kuinua uchumi kwa wakazi wa Manda kupitia huduma watakazozitoa kwa wageni watakaokua wakielekea Mbugani hivyo ametoa shime kwa wakazi hao kujiandaa kutoa huduma mbalimbali kama malazi, bidhaa za utamaduni, vyakula na vitu vingine pindi barabara na daraja hilo vitakapokamilika.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja amewasilisha kero kubwa inayowakabili wakazi wa eneo hilo ambayo kuvamiwa na wanyama pori hususan Tembo ambao huharibu mazao na kutishia maisha yao hivyo amesema kujengwa kwa barabara na daraja eneo hilo kutapunguza kadhia hiyo na kutengeneza fursa kwa Wananchi hao.
Akijibu kero ya Tembo kuvamia Makazi ya watu, Afisa Mfawidhi kutoka Kituo cha TAWA Dodoma Bw. Prosper Kawishe amesema wameagiza vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuwapatia vijana waliopata mafunzo ya kuwadhibiti Tembo hao ili wasiingie kwenye makazi na kuharibu mazao au kuhatarisha maisha ya Wananchi na kipaumbele itakua Kijiji cha Ilangali.
Mbali na kutembelea eneo hilo la mpaka, Mhe. Senyamule ametembelea Mradi wa maji unaotekelezwa na Shirika la 'Water Mission' chini ya ufadhili wa Shirika la 'Charity Water'' katika Kijiji cha Manda unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Milioni 790.7 ambao unatarajiwa kuwanufaisha wananchi 9,921 wa Kijiji hicho huku ukitarajiwa kukamilika June 30, 2025.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa ilihitimishwa kwa kufanya Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Manda ambapo walipata fursa ya kuwasilisha kero zao mbele ya Mhe. Senyamule na Wataalamu alioambatana nao ambapo majawabu ya kero hizo yalipatikana.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.