Na Carlos Claudio, Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametangaza kuwa jumla ya wanafunzi 214,141 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka wa masomo 2025.
Kati ya hao, wasichana ni 97,517 na wavulana 116,624, wakiwemo waliohitimu kutoka shule za Serikali, zisizo za Serikali na watahiniwa wa kujitegemea.
Waziri Mchengerwa amesema wanafunzi 149,818 sawa na asilimia 70, wamepangiwa shule 694 za sekondari za Serikali. Aidha, wanafunzi 1,728 wamepangiwa shule nane zenye ufaulu wa juu zaidi huku wengine zaidi ya 141,000 wakipangiwa shule za bweni na karibu 7,000 wakijiunga na shule za kutwa.
Kwa upande wa vyuo vya elimu ya ufundi, jumla ya wanafunzi 2,875 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vinne vikiwemo ATC, DIT, MUST na WMDI. Pia, wanafunzi zaidi ya 61,000 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya afya, ualimu na kada mbalimbali.
Aidha waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa uchaguzi umezingatia ufaulu na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na mabadiliko ya shule au chuo.
Muhula wa kwanza wa Kidato cha Tano unaanza tarehe 8 Julai 2025, huku tarehe ya mwisho ya kuripoti ikiwa ni 21 Julai.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.