Na Carlos Claudio, Dodoma.
Katika mwendelezo wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kung’ara kwa kutoa elimu na huduma mbalimbali bora za afya kwa wananchi, huku ikisisitiza mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia ya kidigitali.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mkurugenzi wa Huduma Shirikishi wa hospitali hiyo, Dkt. Humphrey Kiwelu, alieleza kuwa wananchi wanaofika kwenye banda la hospitali hiyo wanapata huduma muhimu kama vile usajili, vipimo vya macho, dawa, pamoja na huduma za vipimo vya moyo (ECG na ECHO).
“Hapa tuna huduma mbali mbali za kiafya; kuanzia usajili, kuonana na daktari hadi kupata huduma za vipimo vya moyo. Ni fursa kwa wananchi kufahamu na kufikiwa na huduma hizi muhimu kwa urahisi,”alisema Dkt. Kiwelu.
Aidha, alibainisha kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni miongoni mwa hospitali chache nchini zinazotoa huduma za kibingwa bobezi, ikiwemo matibabu ya magonjwa ya selimundu, huduma za upasuaji wa figo, pamoja na huduma ya kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye matatizo sugu ya figo.
“Tayari tumefanikisha upandikizaji wa figo kwa zaidi ya wagonjwa 53. Huduma hizi kwa sasa zinapatikana hapa nchini, hatua inayosaidia wananchi kuepuka gharama kubwa za matibabu nje ya nchi,” aliongeza Dkt. Kiwelu.
Mbali na huduma hizo, hospitali hiyo sasa inaongoza kwa kutumia mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma zote muhimu – kuanzia usajili wa wagonjwa, kuhifadhi taarifa, kutoa dawa, hadi vipimo vya picha kama X-ray na Ultrasound.
Dkt. Kiwelu amesema mfumo huo umeboresha kwa kiasi kikubwa utoaji huduma kwa kupunguza msongamano na kuondoa tatizo la kupotea kwa mafaili ya wagonjwa.
“Kwa sasa tunatumia mfumo wa kidigitali ambao umeleta mageuzi makubwa. Wagonjwa hawakai muda mrefu kusubiri huduma, na taarifa zao zinapatikana kwa haraka na kwa usahihi. Hatutumii tena makaratasi kama zamani,” alisema.
Kwa kuhitimisha, Dkt. Kiwelu ametoa wito kwa wananchi wote kufika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa na za kisasa, huku akiipongeza serikali kwa kuwezesha huduma hizo kupatikana nchini.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mazingira bora ya utoaji huduma za afya. Kwa sasa Watanzania wengi wanapata huduma bora hapa nchini bila kwenda nje.”
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.