DUWASA YASHIRIKI KWA KISHINDO WIKI YA UTUMISHI WA UMMA, YATOA ELIMU KWA WANANCHI.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kuhudumia wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.


Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la DUWASA, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Aron Joseph, amesema kuwa ushiriki huo unalenga kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kutoa elimu, kusikiliza changamoto, na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira.


“Tumeona ni fursa adhimu kushiriki katika Wiki hii ya Utumishi wa Umma, si tu kwa ajili ya kuonesha mafanikio ya DUWASA, bali pia kusikiliza maoni ya wananchi na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa huduma bora za maji na usafi wa mazingira,” amesema Mhandisi Aron.


Banda la DUWASA ni sehemu ya mwamvuli mkubwa wa Wizara ya Maji, ambapo taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta hiyo zimejumuika ili kuelimisha na kuonyesha huduma mbalimbali zinazotolewa. 


Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Chuo cha Maji, Mfuko wa Maji wa Taifa (National Water Fund), Bonde la Wami Ruvu, RUWASA pamoja na idara mbalimbali za Wizara ya Maji kama Idara ya Ubora wa Maji na Idara ya Rasilimali za Maji.


“Hapa utakapofika katika banda letu, utakuta sekta nzima ya maji ikiwa imeungana pamoja kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kile kinachofanyika ndani ya sekta ya maji. Hii ni fursa nzuri kwa wananchi kuelewa mnyororo mzima wa utoaji wa huduma hizi muhimu,” ameongeza Mhandisi Aron.



Kupitia ushiriki wao kwenye maonesho hayo, DUWASA imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya maji, umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji, pamoja na jinsi wanavyoweza kushirikiana na mamlaka hiyo kuboresha huduma.


Vilevile, mamlaka imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika upanuzi wa huduma, uboreshaji wa mitandao ya usambazaji maji, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, na mipango ya muda mfupi na mrefu inayolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati.


Ushiriki wa DUWASA katika Wiki ya Utumishi wa Umma siyo tu tukio la maonesho, bali ni mwendelezo wa dhamira ya mamlaka hiyo kutoa huduma zenye ubora kwa jamii. Maoni na mrejesho wa wananchi waliotembelea banda hilo yatatumika kama sehemu ya maboresho ya huduma, huku mamlaka ikijipanga kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post