Na Dotto Kwilasa, Dodoma.
Katika vijiji vya wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, idadi ya watoto wanaokosa elimu na haki ya utoto inazidi kuongezeka kila mwaka, huku vichocheo vikuu vikitajwa kuwa ni mila potofu, umaskini na ukosefu wa sheria madhubuti.
Wasichana wadogo wanazidi kushinikizwa kuingia kwenye maisha ya ndoa na mapenzi kabla ya wakati, huku wavulana wakiingia kwenye vishawishi vya ajira zisizo rasmi mijini, wakiachana na ndoto zao za elimu.
Katika kijiji cha Kidoka, baadhi ya ngoma za jando na unyago zimebainika kuwa sehemu ya mafunzo yenye maudhui ya kingono kwa watoto, hali inayosababisha mimba za utotoni, utoro mashuleni na kuvunjika kwa ndoto za baadaye.
Sheikh Salamu Hando, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, anaeleza kwa uchungu jinsi mafundisho hayo yanavyopotosha watoto na kueleza kuwa ;
"Tunaonekana kuwaandaa kwa maisha ya utu uzima, lakini kwa kweli tunawasukuma kwenye maamuzi ya hatari yasiyoendana na umri wao," anasema.
Akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na mradi wa Tuinuke kwa Pamoja unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland Mei 31,2025 Wilayani Chemba amesema jamii inatakiwa kutafuta njia sahihi za kulinda haki za watoto dhidi ya mila zinazowakandamiza.
Arafa Hukomo kutoka kituo cha taarifa na maarifa katika kijiji hicho anaeleza kuwa ukosefu wa sheria kali dhidi ya mila hizo unawaweka watoto wa kike katika hatari ya kupata ujauzito wakiwa bado wadogo.
"Hawakamilishi elimu, wanakatisha ndoto zao mapema, na mara nyingi hubaki kuwa tegemezi kwa familia zao maisha yote," amesema
Ameongeza kuwa kwa upande mwingine, vijana wa kiume hawako salama. Wengi wao huacha shule kwa matarajio ya ‘kujitegemea’ mijini, lakini hujikuta wakifanya kazi duni zisizo na uhakika, huku maisha yao yakidorora kwa kasi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa kijiji hicho, Samalu Lupande, anasema Umaskini wa kaya unalazimisha wazazi kutanguliza maslahi ya muda mfupi. Wengine huona elimu ni gharama isiyo na faida ya haraka.
Anasema baadhi ya watoto wa kike hulaghaiwa kwa misaada ya fedha au mahitaji ya shule kwa masharti ya ngono, jambo linalozidi kuwaumiza kimwili na kisaikolojia.
Amesema kuwa hali hiyo ni hatari si tu kwa mtoto bali kwa taifa zima nankupelekea jamii kuwa na kizazi kilichojeruhiwa .
Vera Assenga kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) amesema si mila zote ni mbaya, lakini ni muhimu kutofautisha kati ya utamaduni na maudhui yenye madhara.
Ametolea mfano wa mila salama kuwa ni pamoja na sanaa ya ngoma, lakini ni lazima kurekebisha mafundisho yake.
Naye Deogratius Temba, mwezeshaji wa mradi wa Tuinuke kwa Pamoja, ameeleza kuwa majadiliano ya wazi ndiyo njia bora ya kuibua mwamko mpya wa kijamii ambapo Watu wanapata nafasi ya kusikia na kujadili bila hofu, ndipo mabadiliko huanza.
Amesema kupitia mdahalo , jamii hupata ujumbe wa kuacha mila zenye madhara ambazo hazipaswi kulindwa kwa jina la utamaduni na badala yake, jamii inapaswa kuweka mbele maslahi ya mtoto, ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kuishi ndoto yake kwa usalama na heshima.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.