Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa wito kwa mamlaka nchini kuanzisha chombo huru cha kudumu cha uchunguzi wa tuhuma dhidi ya vyombo vya usalama, kutokana na taarifa za kutoweka kwa mwanaharakati na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mdude Nyagali, ambazo zimewahusisha baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.
Kupitia chapisho lake katika mtandao wa X, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema haiwezekani vyombo vinavyotuhumiwa, kuchunguza thuma zinazowakabili bila uwepo wa chombo huru kutoka nje ya mfumo wa usalama wa serikali.
"Hakuna kinyozi anaweza kujinyoa, kesi ya Ngedere huwezi mpa Nyani aamue," amesema
Olengurumwa, akisisitiza haja ya kuwa na Civilian Oversight System - tume huru ya kudumu inayojumuisha makundi kama asasi za kiraia, viongozi wa dini, majaji wastaafu na wengine wenye hadhi ya kusimamia haki bila upendeleo.
Olengurumwa ametaja mifano ya nchi zilizofanikiwa kuwa na vyombo hivyo vya uchunguzi kama Kenya yenye Independent Police Investigation Authority (IPOA). Ameeleza kuwa Tanzania haina chombo kama hicho, jambo linaloweka mazingira magumu kwa wananchi kupata ukweli na haki katika tuhuma dhidi ya vyombo vya dola.
Amesema licha ya Tanzania kutokuwa na chombo kama hicho, kwa sasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaweza kutumika kama njia mbadala kwa kuwa na mamlaka ya Ombudsman (Ofisi au mtu wa uchunguzi maalumu). THRDC imeshaiandikia rasmi tume hiyo barua, ikiitaka kuingilia kati na kutumia mamlaka yake ya kisheria kuchunguza tuhuma hizo.
Kauli hiyo imekuja baada ya Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake David Misime kutangaza kuwa limeanzisha uchunguzi maalum dhidi ya askari wake wawili wanaodaiwa kuhusika katika tukio la kutoweka kwa Mdude. Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchunguzi unahusisha kikosi kazi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ambacho tayari kimepelekwa mkoani Mbeya - eneo linalohusishwa na tukio hilo.
Taarifa zilizovuja kwenye mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa mwananchi mmoja alidai kushawishiwa na askari hao kushiriki shughuli za kijajusi kwa ahadi ya malipo, hali iliyozua hisia kali
miongoni mwa wanaharakati.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.