TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA JOPO LA MAWAZIRI KUHUSU MAENDELEO YA UTALII



Na Mwandishi wetu-Tunis, Tunisia.


Sekta ya utalii katika bara la Afrika ni muhimu katika kuendesha uchumi wa nchi mbalimbali ikiwa ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi, kukuza ajira na pia huunganisha nchi jirani kupitia ikolojia mbalimbali ambazo zinafanya kuwepo na juhudi kubwa za uhifadhi wa maliasili na utamaduni.


Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa kwenye mkutano wa Jopo la Mawaziri ambao umefanyika kama sehemu ya Mkutano wa kimataifa wa ufadhili katika uwekezaji na biashara barani Afrika unaoendelea kwenye Hoteli ya Radisson Blu Jijini Tunis, Nchini Tunisia.


Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa jamii nyingi za Afrika zina mazao mengi ya utalii ambayo hayajafanyiwa kazi kwa kutangazwa akitoa mfano hivi karibuni katika nchi ya Tanzania kulifanyika kongamano kubwa la utalii wa vyakula vya asili ambapo wahudhuriaji wengi walionyesha kuvutiwa na vyakula vya asili ambavyo vilionyeshwa katika kongamano hilo.


Katika hatua nyingine Mhe. Kitandula aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Miundo mbinu mbalimbali katika nchi yetu kwenye sekta ya utalii imesaidia kukuza utalii kwa kiwango kikubwa, hivyo ni wakati wa Bara la Afrika kupata uzoefu ya pamoja kwa kuunganisha nguvu ya kutangaza mazao mapya ya utalii kwani kufanya hivyo itaunganisha nchi nyingi kuwa na lugha moja na itachochea utulivu wa kisiasa hivyo kuvutia wawekezaji wengi katika sekta ya Utalii.


Mkutano wa kimataifa wa ufadhilii katika uwekezaji na biashara barani Afrika (FINANCING INVESTMENT & TRADE in AFRICA – FITA2025) ni Fursa kubwa kwa wadau wa Uchumi, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Taasisi za Umma na Binafsi kwani wanapata wasaa wa kukutana na viongozi wa taasisi za kifedha, wafadhili mbalimbali hivyo kupelekea kuwa na mjadala wa pamoja kuhusu changamoto mbalimbali za taratibu za kifedha ili kupata njia bora za kukuza uchumi wa Afrika, kuendesha biashara kati ya nchi na nchi na namna bora ya kufanya uwekezaji wenye tija.





🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post