Mara baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mhe. Tundu Lissu kuhamishwa kutoka Gereza la Keko kwenda Ukonga, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani @exmayor_bonifacejacob amekuwa mtu wa kwanza kumtembelea na kumjulia hali akieleza kuwa Mhe. Lissu amehimiza Wanachama na wafuasi wa Chadema kutokubali kuyumbishwa, akitaka wazidi kupaza sauti kuhusu Kampeni yao ya sasa ya No Reforms, No Election.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jioni ya Aprili 19, 2025 mara baada ya kutoka kwenye mikutano ya Operesheni ya No reforms, No Election inayoendelea kanda ya Pwani, Jacob ameeleza kuwa Mhe. Lissu amemueleza kuwa ni Muhimu kutilia mkazo kwenye kampeni hiyo badala ya kampeni ya kutaka yeye kuachiliwa huru, akieleza kuwa huenda ni ajenda ya Vyombo vya Dola kutaka kunyamazisha kampeni yao ya Kutaka Mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi na sheria zake zisizo na usawa.
"Mwenyekiti yupo vizuri, yupo fiti lakini anasema kampeni ya No Reforms, No election kanda ya Pwani iendelee na anasema mpaka sasa kampeni hiyo bado ipo kwenye njia sahihi." Ameongeza Kiongozi huyo wa Pwani.
Katika hatua nyingine, Boniface Jacob ameeleza kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa @tunduantiphaslissu ameeleza kuwa alipohamishwa Kutoka Keko alielezwa kuwa ni mabadiliko ya kawaida na ndugu, jamaa na marafiki wataendelea kumuona na kumsabahi - badala yake imekuwa tofauti kwani Viongozi wenzake, wanachama na ndugu zake wamekuwa wakizuiwa kwenda
kumsabahi tangu alipohamishiwa Gerezani hapo.
"Kimaisha Ukonga kuna maisha mazuri kuliko Keko kwa maana ya huduma kwasababu pale Ukonga ana room yake binafsi, kule Keko hakuna faragha kwa kiongozi ikiwemo vyoo, si unajua vyoo vya jela havina milango na Mheshimiwa anasema hana shida isipokuwa ameniomba nipaze sauti tu ya kutaka haki yake ya kuruhusiwa watu wake na Viongozi wa Chama kuweza kwenda kumuona Gerezani."
Lissu anayeshtakiwa kwa makosa ya uhaini alikuwa akishikiliwa kwenye Gereza la Keko kabla ya leo taarifa kutoka kuwa amehamishiwa kwenye gereza la Ukonga Dar Es salaam, akisubiri kutajwa kwa kesi yake hapo Aprili 24, 2025 na kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa Chadema anatarajiwa kusherehekea sikukuu ya Pasaka akiwa mahabusu