Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakisha Hospitali zote nchini zinakuwa na wodi maalumu za watoto.
Dk.Samia ametoa maagizo hayo hii leo Oktoba 28, 2023 wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria kwa mwaka 2022 na ugawaji wa magari ya kubebea wagonjwa na vifaa tiba katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Rais Samia emesema Wizara na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zihakikishe wodi hizo zinakuwa na watumishi wenye ujuzi,vifaa tiba na dawa muhimu kwa watoto hao wachanga.
Rais Samia pia amezitaka Wizara ya Afya,TAMISEMI na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kushirikiana kubeba ajenda ya kupambana na udumavu wa watoto chini ya miaka 5 na kuiwekea mpango wa utekelezaji.
Dk.Samia amezitaka Wizara hizo kupanua wigo wa uelemishaji na uhamasishaji wa masuala ya lishe ili kupunguza zaidi kiwango cha udumavu nchini ambacho kimepungua kutoka 34% mwaka 2015/16 hadi 30% mwaka 2022.
Sanjari na hayo Dk.Samia amesema matokeo chanya yaliyobainishwa na utafiti huu yamedhiirisha matokeo ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali katika sekta ya afya.
Aidha Dk.Samia amegawa seti 120 za vifaa vya huduma kwa watoto wachanga na wenye uzito pungufu,mashine 125 za mionzi,mashine 140 za kutibu dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi ambavyo vitasambazwa kwenye hospitali za Halmashauri na vituo mbalimbali vya afya kote nchini.