Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kisasa,nyumba za watumishi na uchakavu wa vituo vya kutolea huduma za afya.
Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo Oktoba,28 mwaka huu wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya mareria Tanzania ya mwaka 2022 na ugawaji wa magari ya wagonjwa na vifaa tiba iliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es salaam.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Septemba 2023 idadi ya zahanati zinazotoa huduma za afya zimeongezeka kutoka zahanati 4127 hadi zahanati 5646 ambapo vituo vilivyosajiliwa na kutoa huduma vimeongezeka kutoka vituo 535 hadi kufikia 788.
Mhe.Mchengerwa alisema vituo vinavyotoa huduma ya upasuaji vimeongezeka kutoka vituo 115 hadi kufikia vituo 537 ifikapo Septemba 2023huku akisema jumla ya hospitali mpya zilizojengwa katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita ni 119 wakati 18 zimekarabatiwa pamoja na kupanuliwa.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 na 2022/2023 Ofisi ya Rais TAMISEMI imetumia kiasi cha fedha takribani Bilioni 194.48 katika kuboresha miundombinu ya afya ya msingi na upatikanaji wa vifaa ambapo yamejengwa majengo 83 ya dharura,majengo 28 ya wagonjwa mahututi na kituo cha matibabu wakati nyumba zilizojengwa ni 150 ununuzi wa vifaa tiba na mitambo ya kuzalisha hewa tiba kwenye halmashauri 13 mashine za mionzi 137 magari 316 na pikipiki 517.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili serikali imetoa Shilingi Bilioni 368.12 kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 165.15 zilitolewa katika kipindi cha mwaka 2021/22 ili kutekeleza huduma za afya nchini.
Mhe.Mchengerwa alisema maboresho ya miundombinu yanakwenda sambamba na upatikanaji wa rasilimali watu ambapo Ofisi ya Rais Tamisemi imeajiri watumi wa kada za afya 17,950 kwa katika kipindi cha miaka miwili.
Mhe.Mchengerwa amewaagiza wakuu wa mikoa kufungua vitua hivyo ili kutoa huduma kwa wananchi huku akiwataka watumishi waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi kuhakikisha wanatoa huduma na lugha nzuri kwa wateja.
“Nitahakikisha nachukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote watakaobainika kuzembea katika kuwahudumia wananchi.
“Jukumu la usimamizi wa utoaji wa huduma ni jukumu la kila mmoja wetu nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wanaofuata huduma kutosita kutoa taarifa za watumishi wasio waadilifu,wazembe na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo,”alisema Mhe.Mchengerwa