Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya Tanzania na Ujerumani zimekubaliana kuwa na mazungumzo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwaka 2024.
Serikali hizo zimeagiza timu kutoka pande zote mbili kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara yanayolenga kuimarisha ushirikiano na kubainisha maeneo mapya yenye umuhimu kwa nchi zote mbili.
Rais Samia amesema hay oleo Oktoba,31,mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumpokea na kuzungumza na Rais wa Shirikisho la Ujerumani Dkt.Frank Walter Stainmeier ambaye yupo nchini kwa ziara yake ya kikazi ya siku tatu.
Aidha Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania ikotayari kufungua majadiliano kuhusu yaliyopita kwenye Historia ya utawala wa Ujerumani ambapo mojawapo ni urejeshaji wa mabaki yaliyopo kwenye makumbusho mbalimbali ya Ujerumani kwa familia zao.
Rais Samia anatambua juhudi za pamoja zinazofanywa na taasisi za Serikali hizo mbili zinazolenga kufanikisha azma huyo ikiwemo pia kuwajengea uwezo wa taaluma na kuongeza uwezo wa makumbusho za Tanzania na Ujerumani.
Rais Samia pia ameishukuru Ujerumani kwa namna inavyounga mkono Tanzania kwenye miradi ya maendeleo hususani sekta za afya,maji,kilimo,elimu,utalii,utamaduni,michezo,ulinzi,maliasili,uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa fedha.
Hata hivyo kuhusu uwekezaji Dk.Samia amesema viongozi wote wawili wamekubaliana na kusisitiza mchango muhimu wa biashara na uwekezaji katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.