Na Fedrick Mbaruku
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kuhakikisha mapato na matumizi yatokanayo na mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi yanatengwa na yanatumika katika sekta husika kulingana na miongozo iliyopo kuboresha sekta hizo.
Waziri Mkuu ametoa wito huo Agosti mwaka huu wakati akizungumza na wadau na washiriki mara tu baada ya kukagua mabanda ya maonesho ya Nane nane yanayoendelea katika viunga vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Amesema serikali inaendelea kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za kifedha ili ziweze kushusha riba kwenye mikopo wanayotoa na kuongeza fursa kwa wajasiliamali nchini ili wapate mikopo na kuendeleza shughuli zao ziweze kuwa na tija.
“Taasisi za fedha zimefungua dirisha kwa ajili yenu wanataka wawasikie hakuna maendeleo bila kukopa lakini ni lazima vigezo na masharti vizingatiwe unapotaka kufanya maendeleo na hauna mtaji nenda kakope lakini ukikopa ni lazima uresheje ili na wengine wakakope.
“Ofisi ya Rais (TAMISEMI) hakikisheni mnasimamia miongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2023/2024 unaozitaka mamlaka za serikali za mitaa kutenga mapato ya nchi yanayotokana na tozo mbalimbali kwenye mazao kilimo(Asilimia 20) mifugo (Asilimia 15) na uvuvi (Asilimia 5) zinarudi na kutumika kuboresha sekta hizo.
Aidha Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Serikali za mitaa nchini kushirikiana na wizara husika kuhakikisha vijana wanapatiwa maeneo ya mashamba na mafunzo na kuwatafutia wadau watakaowasaidia kupata mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo,mifugo,uvuvi na masoko ya uhakika.