Papa Francis amewataka waamini wakanisa katoliki Duniani kote kujitakasa kwa unyenyekevu na kwa muda mrefu ili kukabiliana na kilio cha uchungu cha waathirika wa unyanyasaji wa kingono waliotendewa na makasisi.
Papa huyo alikutana na kuzungumza na waathirika hao kwa faragha jana Jumatano katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Ureno.
Papa Francis alikuwa akizungumza mjini Lisbon mwanzoni mwa ziara ya siku tano nchini humo ambayo anatumai itawahamasisha vijana wa kikatoliki wakati wa siku ya vijana duniani, tamasha kubwa zaidi la kikatoliki duniani.
Inaelezwa kuwa miezi sita iliyopita, ripoti ya tume ya Ureno ilisema takriban watoto 4,815 walinyanyaswa kingono na makasisi kwa zaidi ya miongo saba.
Mzozo huu “unatuomba kujitakasa kwa unyenyekevu kwa muda mrefu, tukianza na kilio cha uchungu cha waathirika, ambao lazima wakubaliwe na wasikilizwe kila mara,” Francis alisema katika hotuba yake kwa maaskofu, mapadre na watawa katika ibada ya jioni ndani ya makazi ya watawa.
Francis alikutana kwa faragha na waathirika 13 walionyanyaswa kingono katika ubalozi wa Vatican mjini Lisbon jana Jumatano jioni, huku Vatican ikisema katika taarifa kwamba mkutano huo ulifanyika katika “mazingira ya usikilizaji mkubwa” na ulidumu kwa zaidi ya saa moja.