WAKATI Dunia ikiadhimisha Wiki ya unyonyeshaji iliyoambatana na kaulimbiu isemayo “Saidia unyonyeshaji wezesha wazazi kulea na kufanya kazi zao za kila siku”akinamama wajawazito na wanaonyonyesha wametakiwa kuzingatia suala la usafi na kutenga muda wa kupumzika ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto mara tu baada ya kujifungua.
Akitoa elimu katika semina iliyofanyika Agosti,01, mwaka huu katika Kituo cha afya Makole kilichopo Jijini Dodoma,Mratibu wa Rishe Jijini Dodoma Semeni Juma amesema kaulimbiu hiyo inaenda sambamba na uboreshaji wa afya ya mama na mtoto.
Amesema kumekuwa na changamoto ya rishe kwa akina mama wajawazito na wanaoonyonyesha ambapo amesema tangu mwaka 2011 serikali imeweka mikakati thabiti katika halmashauri zote nchini ili kuratibu masuala ya rishe katika ngazi ya halmashauri ikiwa ni pamoja na kuwapa vipaumbele Watoto walio na umli wa miaka 5, wamama wajawazito na wanaonyonyesha na vijana walio katika rika ya barehe.
“Serikali imeweka mikakati muhimu sana ili kuhakikisha haya makundi maalumu yanakuwa katika hali nzuri ya ukuaji,lakini si tu kwa hao kwa maana ya kwamba wengine hawana umuhimu hiyo ni kwa sababu ya hatua mbalimbali za ukuaji lakini mama mjamzito na anaenyonyesha anamahitaji mala mbili Zaidi ya mtu mwingine kwahiyo Akina baba nao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kufika vituo vya afya na kuchunguza afya ya mama kabla hajajifungua ili kupatiwa elimu itakayosaidia kulinda afya ya mama na mtoto.
Aidha Mratibu huyo amewashauri akinamama hao kutumia vyema simu janja katika kusoma njia sahihi za unyonyeshaji,kuwatumia wataalamu mbalimbali wa afya,pamoja na kuhudhuria kriniki mara kwa mara huku akiwataka akina Baba kuwasaidia akinamama na kusema mama anaenyonyesha ikiwa atakumbwa na msongo wa mawazo kiwango cha uzalishaji wa maziwa ya mtoto hupungua na mawasiliano ya kisayansi kukata.
Nae Mganga Mkuu Mkoa wa Dodoma Dr.Endlu Methwi amesema akina mama wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba Watoto wananyonyeshwa ipasavyo hususani katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
Hata hivyo amewasihi akina mama wajawazito na wanaonyonyesha kuwapa Watoto maziwa ya mama pekee huku akieleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mtoto akinyonya maziwa ya mama peke yake katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo anakuwa na uwezo mkubwa wa kiakili,uwezo wa kupambanua mambo,uwezo wa kufikilia na uwezo wa kufanya maamzi anapokuwa mkubwa.
“Kwahiyo Watoto ambao wamenyonyeshwa maziwa ya mama peke yake kwa miezi sita ukilinganisha na Watoto ambao hawajanyonyeshwa kwa muda kama huo kumekuwa utofauti katika ukuaji wao na ndiomaana tunasisitiza na kuwahamasishwa akina mama kuhakikisha wanazingatia taratibu za unyonyeshaji mara tu baada ya kujifungua.
“Hivyo nichuku nafasi hii kuwataka wananchi na wakazi wa Mkoa wa Dodoma tuhakikishe tunazingatia taratibu za unyonyeshaji na pia tuangalie sio kunyonyesha tu kuna taratibu za kunyonyesha na pia kuna taratibu za kumshikilia mtoto anapotaka kuanza kunyonya,”amesema Dr.Methwi
Pamoja na hayo akinamama hao nao wameoneshwa kufurahishwa na elimu waliyoipa katika maadhimisho hayo ambapo wamesema wataendelea kufuata njia sahihi za kunyonyesha na kuwashirikisha waume zao katika suala zima la makuzi ya mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama.