Na Fedrick Mbaruku
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule amewataka wadau mbalimbali kujitokeza katika maonesho ya siku ya wakulima (Nane nane) ambayo hufanyika Agosti,8 kila mwaka yanayotarajia kuanza Agosti, 01.2023.
Mhe.Senyamule aliyasema hayo Agost,31, mwaka huu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Mhe.Senyamule alisema katika kanda ya kati inayohusisha mikoa ya Dodoma na Singida imepewa dhamana ya kuhakikisha sherehe za wakulima zinafanyika kwa ufanisi.
Alisema katika maonesho ya mwaka huu Mikoa hiyo imejipanga kuongeza hamasa ya kuzalisha kwa tija ambapo kutakuwa na teknolojia mbalimbali za kuongeza tija zitakazochochea mnyororo wa thamani,wadau kupata fursa za kubaini teknolojia zitakazoongeza tija katika uzalishaji wao pamoja na kusambaza mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na uharibifu wa mazingira.
"Mikoa ya Dodoma na Singida imeendelea kuathiliwa na mabadiliko ya tabia ya nchi na hivyo kuathili uzalishaji wa mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi.
"Maonesho ya mwaka huu yameandaliwa ili kutoa ujumbe utakao wapa hamasa wafugaji,wakulima na wavuvi kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa maji,udongo mashambani zikijumuisha matumizi ya makinga maji,kilimo cha jembe tisa na jembe la mzambia,lakini pia kuzalisha mazao yanayotumia maji kwa ufanisi hususani mtama na alizeti,uzalishaji wa malisho ya mifugo,hifadhi ya misitu na upandaji wa miti pamoja na matumizi ya nishati mbadala(Umeme na Gesi),"Mhe.Senyamule
Aidha Mkuu huyo alisema maonesho hayo yatatumika kuhamasisha vijana katika kujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo,mifugo na uvuvi huku akizitaka halmashauri kuwa vinala wa kuwahamasisha vijana waliofanikiwa kuonyesha namna walivyonufaika huku akipigia mfano BBT.
Alisema katika maonyesho ya mwaka huu makampuni ya watu binafsi yameleta teknolojia bora za ufugaji,mbegu bora za mazao mbalimbali vilivyozingatia vipaumbele vya mikoa ya Dodoma na Singida na kusema taasisi za kiutafiti katika sekta za kilimo,ufugaji na uvuvi zinashiriki maonyesho hayo ili kuonyesha teknolojia mbalimbali zilizoanzishwa kwenye vituo vya utafiti na kuwawezesha wakulima kunufaika na elimu ya uzalishaji bora.
Alisema matukio muhimu katika maadhimisho yam waka 2023 yatakuwa na utofauti kwa kuhusisha matukio muhimu na makongamano yatakayo panua wigo wa uzalishaji bora likiwepo kongamano la tasnia ya alizeti huku akisema Mikoa ya Dodoma na Singida ilikabidhiwa dhamana ya kuzalisha zao la alizeti kwa wingi ili kupunguza naksi ya mafuta ya kupikia nchini hivyo hali hiyo itasaidia kuokoa fedha za kigeni zinazotumika katika uagizaji wa mafuta ya kupikia nje ya mipaka ya Tanzania.
Mhe.Senyamule alisema mikoa hiyo iliandaa mikakati ya utekelezaji wa kuhakikisha kunakuwepo kunaongezeko la mafuta kupikia na bei kushuka kutoka shilingi 7000/= kwa lita ambapo hadi sasa wasitani ni shilingi 4000/= kwa lita moja ya mafuta.
Alisema maonyesho hayo yanatarajia kutanabaisha munyororo mzima wa tasinia hiyo katika eneo maalumu ndani ya uwanja litakalopewa jina la mtaa wa alizeti ambapo kutakuwa na mada na maelezo maalumu muhimu kuhusiana na uzalishaji wa zao la alizeti,matumizi ya mbegu bora na maandalizi sitahiki ya mashamba huku akisema zao la mtama litapewa uzito kutokana na kustahimili hari ya hewa katika ukanda huo.
Mhe.Senyamule alisema Wizara ya mifugo imegundua teknolojia ya uimishaji wa kuku wa kienyeji itakayosaidia katika ongezeko la uzalishaji wa kuku hao wanaopenda na kuhitajika na walaji wengi wa nyama ya kuku.
Sanjari na hayo Mhe.Senyamule alisema maonyesho hayo yatawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo,watafiti,wafanyabiashara,wafugaji,wamiliki wa Hoteli,migahawa na super market ili kujadili fursa zitakazosaidia kukuza sekta hiyo na kuchangia ukuaji wa uchumi,usalama wa chakula pamoja na uimalishaji wa lishe katika jamii.