WIZARA YA ARDHI YAPEWA SHILINGI BILIONI 82.13 KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI

Na Fedrick Mbaruku

Serikali imeipa Wizara ya Ardhi kiasi cha fedha shilingi Bilioni 82.13 sawa na asilimia 203 zitakazotumika kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na makazi Dkt.Angelina Mabula Juni 25 mwaka katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mhe.Daniel Chongolo katika Uwanja wa Mtekelezo Jijini Dodoma.

Dkt.Mabula amesema wananchi wanatakiwa kuendelea kutunza ardhi na kujua sehemu sahihi ya kuwasilisha kelo zao zinazohusiana na masuala ya ardhi kutokana na tabia ya baadhi ya wananchi kupeleka malalamiko yao katika ngazi za juu bila kupitia ngazi za chini. 

Dkt.Mabula amewataka Mamlaka za upangaji,Mamlaka za mipango miji na Madiwani nchini kote kutekeleza wajibu wao na sio kuwa madalali wa viwanja ambapo amesema nao wanachangia katika ongezeko la migogoro hiyo.

Amesema kwa hatua za awali wizara hiyo imetembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni hatua ya kutatua migogoro ya ardhi ipatayo 975 nchini.

Amesema hadi sasa wizara hiyo imefanikiwa kutembelea maeneo yote ikiwemo Dodoma huku ikitafuta aina na chanzo cha migogoro hiyo ili kuona hatua za kuchukua kupitia mamlaka husika.

Dkt.Mabula amesema katika kutatua migogoro hiyo wizara imejipanga vyema kuwa na makamishina wawili ambapo mmoja atashughulika na migogoro ya ardhi ndani ya Jiji la Dodoma huku mwingine akitarajia kupewa jukumu la migogoro iliyoko pembezoni mwa Jiji na Wilaya kwa ujumla.

Amesema migogoro iliyopo ni mingi hali ambayo imelazimu kuongeza makamishina ili kuweka na kuongeza nguvu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Pamoja na hayo amesema kuwa wizara imeunda kamati itakayozunguka katika kata nane la Jiji la Dodoma na kuweza kubaini migogoro yote ambapo kati ya maeneo yatakayofikiwa na kamati hiyo ni Nkonze ambapo watu 109 waliwasilisha kelo zao na kusikilizwa,Ipagara 101,Makulu 209,Nzuguni 147,Chawa 9,Miuji 53 na Kizota 60.

Hata hivyo Dkt.Mabula amesema changamoto inayowakabili wananchi ni kutokuwa na uelewa namna ya kuwasilisha na kuweza kutatuliwa migogoro yao kwa madai ya wengi kukimbilia wizarani.

“Wengi wamekuwa wakikimbilia wizarani matokeo yake mnaleta hija wizarani ili mimi niweze kuitatua lazima nirudi kule chini niweze kujua maelezo yake ya msingi niwaombe wana Dodoma pale unapopata changamoto usikimbilie ngazi ya juu anzia ngazi ya chini pale ulipo tunajua mtendaji kata yupo,tuna afisa tarafa,tuna mkurugenzi,tuna mkuu wa wilaya lakini pale unapoona unazungushwa ofisi ya wizara ikowazi kwa sababu kunamaeneo mukienda hampati fursa ya kuonana na viongozi ndiomaana hapo nyuma Dodoma kuongea na mkurugenzi ilikuwa ni kama kumuona Rais Samia,”Dkt.Mabula

Previous Post Next Post