WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) MHE.ANGELLAH KAIRUKI ATOA UFAFANIZI KWA WAAJIRIWA WAPYA NCHINI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Angellah Kairuki amesema upangaji wa watumishi wa ajira mpya ya kada za Afya na Ualimu katika vituo vya kutolea huduma za Afya na Shule umezingatia maombi ya watumishi katika Halmashauri husika.

Waziri Kairuki ameyasema hay oleo Juni 5,2023 alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi za TAMISEMI Jijini Dodoma.

Waziri Kairuki amesema waajiriwa wapya wanatakiwa kuripoti katika Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri huku wakiwa na viambatanishi kikiwemo kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho wa NIDA,Cheti halisi cha kuzaliwa,Vyeti halisi vya kidato cha Nne,Sita,Chuo Kikuu,NACTE,Leseni haina Vyeti halisi vya Mabaraza ya Kitaaluma ili kuhakikiwa na mwajiri kabla ya kupewa barua ya uajiri.

“Mtakumbuka mwezi April 2023 Mhe.Dk.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa kibari cha ajira kwa watumishi 21,200 kati yao 13,130 walikuwa wa kada ya ualimu na 8,070 wa kada ya Afya.

“Baada ya kupata kibari cha ajira Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitoa taangazo kwa wahitimu mbalimbali kwa Walimu na kada za Afya kuwasilisha maombi ya kazi kupitia mfumo wa kielektroniki kupokea na kuchakata maombi ya ajira kuanzia tarehe 12/04/2023 hadi 25/04/2023.

Waziri Kairuki amesema jumla ya maombi 171,916 yakiwemo ya wanawake 76,190 na wanaume 95,726 yaliyopelekwa kwenye mfumo ambapo maombi ya kada za afya yalikuwa ni 48,705 na kada ya ualimu ikiwa ni 123,211.

Pia Waziri Kairuki amebainisha kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI iliunda timu maalumu ya uchambuzi ambayo ilifanya kazi ya kuchambua na kuhakiki maombi mbalimbali ya ajira ambapo uhakiki huo ulifanyika katika hatua mbalimbali kutokana na idadi ya waombaji kuwa kubwa.

Amesema timu hiyo iliainishiwa vigezo vya kuzingatia katika mchakato wa uchaguzi wa waombaji ajira ili kuhakikisha kunakuwepo na haki na uwazi katika zoezi hilo ikiwa ni pamoja na mwaka wa kuhitimu kikiwa ni kigezo kilicho zingatiwa,kigezo cha umli wa kuzaliwa, pamoja na uchambuzi wa watu wenye ulemavu.

Amesema mchakato wa uhakiki na uchambuzi wa kada za afya na ualimu ulifanywa kwa awamu mbili ambapo uhakiki wa awali ulifanywa kwa mufumo na kati ya maombi 171,919 yaliyopokelewa,waombaji 49,089 waliondolewa kwenye mchakato hali iliyofanya kubaki na waombaji 122,827.

Hata hivyo ameeleza kuwa waombaji walioondolewa awali ni 1456 waliomba nafasi za ualimu wakiwa wamehitimu kabla ya mwaka 2015 huku waombaji 47,633 waliomba masomo ambayo hayakutangazwa katika matakwa ya tangazo la ajira.

Sanjali na hayo katika uhakiki wa awamu ya pili ulihusisha uhakiki wa nyaraka zilizoambatananishwa kwenye maombi ya muombaji ikiwemo cheti cha elimu ya kidato cha nne,sita,Chuo Kikuu ambacho muombaji amejipatia taaruma pamoja na cheti cha kuzaliwa.

Pamoja na hayo Waziri Kairuki amesema baada ya zoezi la uhakiki wa waombaji wa kimfumo na mapitio ya nyaraka jumla ya waombaji 86,448 walikidhi vigezo na hivyo kuingizwa katika mchakato wa kupangiwa vituo vya kazi ambapo kati ya waombaji 86,448 waliokidhi vigezo waombaji wa kada za afya ni 21,273 ambapo kati yao wanawake ni 10,618 na wanaume ni 10,655.

Amesema waombaji wa kada za elimu ni 65,175 walikidhi vigezo ambao kati yao wanaume ni 38,584 na wanawake ni 26,591.

“Waombaji 86,448 waliokidhi vigezo na sifa walitakiwa kujaza nafasi za kazi 21,200 walimu 13,130 na afya ni 8,070 kwa mjibu wa kibali kilichotolewa,”Waziri Kairuki

Aidha amesema kwa waajiriwa wapya watakao chukua posho ya kujikimu na baadae kukiuka kuripoti katika maeneo yao ya kazi waliyopangiwa watachukuliwa hatua stahiki kwa mjibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kushitakiwa kwa kosa la kujipatia fedha au mali kwa njia ya udanganyifu.

 

 

 

 

Previous Post Next Post