Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imeendelea kuongeza nguvu katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini, ambapo hadi sasa imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. trilioni 1.55 kwa ajili ya kufadhili miradi 862 ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imewafikia zaidi ya Watanzania milioni 2.6 kupitia huduma za mikopo na uwekezaji, huku zaidi ya wakulima wadogo 657,000 wakinufaika kupitia mikopo iliyotolewa kwa kushirikiana na benki 21.
Akizungumza Agosti 8, 2026 katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Nyabundege amesema Sh. bilioni 692 zimetolewa kupitia benki hizo 21 kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo kupata mitaji na kuongeza uzalishaji.
Amesema kati ya mikopo yote iliyotolewa na TADB, kiasi cha Sh. trilioni 1.32, sawa na asilimia 84, kimetolewa katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Nyabundege, mafanikio hayo yameenda sambamba na ongezeko la mtaji wa benki hiyo kutoka Sh. bilioni 60 mwaka 2021 hadi Sh. bilioni 452 hivi sasa, hatua inayoiwezesha TADB kuongeza uwezo wa kutoa fedha kwa shughuli mbalimbali za kilimo.
Amesema fedha hizo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, pamoja na ujenzi wa mifumo ya umwagiliaji, maghala, vihenge na viwanda vya uchakataji, kwa lengo la kuongeza tija na thamani ya mazao ya wakulima.
“Fedha hizi zimefika mashambani, kwenye miradi ya mifugo na uvuvi, zimejenga mifumo ya umwagiliaji, maghala, vihenge na viwanda vya uchakataji, na hivyo kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko,” amesema Nyabundege.
Katika kuimarisha uzalishaji wa chakula nchini, TADB imesema imewekeza Sh. bilioni 611.8 katika mazao ya chakula pekee, huku sekta za kimkakati zikiwemo mafuta ya kula, kahawa, korosho, sukari na pamba zikipatiwa uwekezaji wa jumla ya Sh. bilioni 884.24.
Nyabundege amesema TADB itaendelea kuongeza kasi ya ufadhili katika sekta ya kilimo ili kuchochea uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kutengeneza ajira na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Amesema hatua hiyo pia inalenga kusaidia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususan katika kujenga sekta ya kilimo yenye tija, ushindani na uwezo wa kuleta maendeleo kwa wananchi.
