FDH, STAMICO NA CHUO CHA MAFUNZO ZANZIBAR, KUSAINI MAKUBALIANO YA KIHISTORIA YA USAMBAZAJI MKAA MBADALA


Na Carlos Claudio, Dodoma. 📍


Foundation for Disabilities Hope (FDH) kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Chuo cha Mafunzo Zanzibar,, kesho Agosti 11, 2026, wanatarajia kusaini makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha usambazaji mkubwa wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquette, hatua inayolenga kuimarisha matumizi ya nishati safi na kupunguza athari za matumizi ya nishati chafu. 


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amesema tukio hilo ni la kihistoria kwa kuwa linafungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika kukuza matumizi ya nishati safi nchini. 


Salali amesema FDH imepewa jukumu la kuwa wakala mkubwa wa uuzaji wa mkaa huo mbadala na kwamba taasisi hiyo imekuwa ikifanya mazungumzo na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia wananchi kwa wingi.


 “Kesho tutakuwa na tukio kubwa la kihistoria la kusaini makubaliano ya ushirikiano baina ya Chuo cha Mafunzo Zanzibar na STAMICO, kwa kushirikiana na FDH, katika usambazaji mkubwa wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquette,” amesema. 



Amesema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuhifadhi mazingira, huku akieleza kuwa mkaa mbadala wa Rafiki Briquette unalenga kuwasaidia Watanzania kupunguza utegemezi wa nishati zinazochangia uharibifu wa mazingira. 


Kwa mujibu wa Salali, FDH imepata heshima ya kuwa miongoni mwa wasambazaji wa mkaa huo baada ya kukabidhiwa cheti cha uwakala, jambo alilosema limeipa taasisi hiyo msukumo wa kuhakikisha agenda ya nishati safi inatekelezwa kwa vitendo. 


Amesema ushirikiano huo kati ya Chuo cha Mafunzo Zanzibar, STAMICO na FDH utasaidia kuongeza upatikanaji wa mkaa mbadala na kuwawezesha wananchi kutumia nishati rafiki kwa mazingira. 


“Tunajivunia sana utekelezaji wa agenda hii ya nishati safi na tunajivunia STAMICO kwa kuja na mkaa mbadala ambao unaenda kusaidia utunzaji wa mazingira na kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati chafu,” amesema. 



Salali pia ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na kujenga mazingira bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo. 


Amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo kesho kutakuwa mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano katika usambazaji na matumizi ya nishati safi, huku akisisitiza kuwa FDH iko tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquette unapatikana kwa wananchi kwa urahisi. 


Tukio hilo linatarajiwa kufungua fursa mpya ya usambazaji wa mkaa mbadala kwa wigo mpana, sambamba na kuunga mkono juhudi za kitaifa za kulinda mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.








Previous Post Next Post