Dodoma.📍
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini kupitia utoaji wa huduma za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafugaji na wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo kuongeza uzalishaji na tija.
Mhe. Chande ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TADB katika Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nanenane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Amesema TADB imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kuendeleza kilimo kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima na wawekezaji wa sekta hiyo, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
"Taasisi kama TADB zina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuinua sekta ya kilimo. Uwezeshaji wa kifedha unaotolewa na benki hii unawapa nguvu wakulima na wafugaji kuongeza uzalishaji na kutumia fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo," amesema Mhe. Chande.
Akiwa katika banda hilo, Naibu Waziri alipatiwa maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TADB, ikiwemo mikopo kwa wakulima, wafugaji na wawekezaji wa sekta ya kilimo, pamoja na programu maalumu zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali wa kilimo.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kuziunga mkono taasisi zinazowekeza katika maendeleo ya kilimo, akibainisha kuwa sekta hiyo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania na chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa wananchi wengi.
Maonesho ya Nanenane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha teknolojia, huduma na ubunifu unaochochea maendeleo ya sekta ya kilimo, huku TADB ikiendelea kutumia fursa hiyo kutoa elimu na huduma za kifedha kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

