CHANDE AIPONGEZA WMA KWA KUTOA ELIMU YA VIPIMO KWA WANAFUNZI


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, ameipongeza Wakala wa Vipimo (WMA) kwa juhudi zake za kutoa elimu ya vipimo kwa wanafunzi, akisema hatua hiyo inasaidia kujenga kizazi chenye uelewa wa umuhimu wa vipimo sahihi katika biashara na maisha ya kila siku.


Mhe. Chande ametoa pongezi hizo leo, Agosti 6, 2026, alipotembelea banda la WMA katika Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.


Akiwa bandani hapo, Naibu Waziri huyo alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi waliokuwa wamepatiwa elimu kuhusu vipimo na kuwahoji maswali mbalimbali, ambapo alifurahishwa na uwezo wao wa kujibu kwa ufasaha na kuonesha uelewa mkubwa wa elimu waliyopewa.


Mhe. Chande alisema ni hatua muhimu kwa WMA kuanza kuwajengea watoto uelewa kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi wakiwa katika umri mdogo, jambo ambalo litawasaidia kuwa walaji na wafanyabiashara wenye uelewa katika siku zijazo.


“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa wameelewa kuwa kipimo sahihi ni haki ya kila mtu. Hawa ndio Maafisa Vipimo wa kesho,” alisema Mhe. Chande.


Wanafunzi hao kutoka Shule ya Msingi Blessed Mabuba ya jijini Dodoma waliongozana na mwalimu wao, Irene Ketta, ambaye pia aliipongeza WMA kwa kupeleka elimu ya vipimo kwa wanafunzi na mashuleni.


Mwalimu Ketta alisema elimu hiyo imewawezesha wanafunzi kuelewa tofauti kati ya kipimo sahihi na kisicho sahihi, umuhimu wa kusoma lebo za bidhaa pamoja na namna sahihi ya kutumia mizani.


“Niwape pongezi WMA. Kama tutaendelea kuwapa elimu hii watoto wetu, tunajenga Taifa la wafanyabiashara waaminifu na walaji wenye ufahamu. Huu ndio msingi wa uchumi imara,” alisema Mwalimu Ketta.


Kwa upande wake, WMA imeahidi kuendelea kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wanafunzi, ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika kulinda haki za walaji na wafanyabiashara.

Previous Post Next Post