WAZIRI WA FEDHA AHAMASISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LA TOST SABASABA

 


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewahimiza wananchi na wafanyabiashara kutembelea banda la Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na ofisi hiyo.


Rai hiyo imetolewa Julai 2, 2026, wakati Waziri Omar alipotembelea banda la TOST lililopo ndani ya Jengo la Wizara ya Fedha katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Amesema wananchi na wafanyabiashara wanapaswa kutumia fursa ya maonesho hayo kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya TOST, pamoja na namna ofisi hiyo inavyopokea, kusuluhisha na kufuatilia malalamiko au taarifa zinazohusu masuala ya kodi.



“Huduma zinazotolewa na TOST zina mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, kuboresha mazingira ya biashara na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Waziri Omar.


Kwa upande wake, Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Bw. Erastus Mtui, amesema ofisi hiyo imeweka kambi katika maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kuhusu haki na wajibu wao katika masuala ya kodi.


Amesema TOST pia inapokea malalamiko na taarifa za kodi kutoka kwa wananchi na kuzifanyia kazi kwa wakati kwa mujibu wa sheria, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya walipakodi na mamlaka husika.


Bw. Mtui amesema utoaji wa elimu na usuluhishi wa malalamiko ya kodi utasaidia kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini.



🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post