UKIJA SABASABA USIBEBA CASH, YAS YAHAMASISHA MALIPO YA KIDIJITALI


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Kampuni ya mawasiliano ya YAS imewahamasisha wananchi wanaotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba kutumia huduma za malipo ya kidijitali badala ya kubeba fedha taslimu, ili kurahisisha manunuzi, malipo ya viingilio na miamala mingine mbalimbali.


Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la kampuni hiyo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba jijini Dar es Salaam, mwakilishi wa YAS alisema kampuni hiyo imefika katika maonesho hayo kwa kaulimbiu isemayo, “Ji Mix Kibiashara Sabasaba.”


Alisema kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kutambua umuhimu wa kufanya malipo kwa njia za kidijitali, hususan wanapofanya manunuzi au kupata huduma mbalimbali ndani ya viwanja vya maonesho.


“Tunawaambia wananchi kuwa ukija Sabasaba usibebe cash mkononi. Tumia wakala, huduma za benki au mifumo mingine ya malipo ya kidijitali ili ufurahie huduma kwa urahisi zaidi,” alisema.



Aliongeza kuwa matumizi ya malipo ya kidijitali yanaweza kumsaidia mteja kufanya malipo ya kuingia getini, kununua bidhaa na kupata huduma mbalimbali kwa haraka, salama na kwa urahisi zaidi.


Kwa upande wake, huduma ya Mixx imeeleza kuwa ipo kwenye maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wateja, wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na bidhaa na huduma zake.


Mwakilishi huyo alisema wafanyabiashara wanaofika katika banda hilo wanaweza kupata huduma ya Lipa Namba kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji wa malipo kutoka kwa wateja wao, pamoja na vitendea kazi vinavyowasaidia katika shughuli zao za kila siku.


Alisema mawakala na wajasiriamali pia watapatiwa maelekezo kuhusu taratibu za kujiunga na huduma hizo na namna ya kuzitumia kwa ufanisi katika kukuza biashara zao.


Aidha, alisema wafanyabiashara wakubwa wanaweza kunufaika na mfumo wa Mixx Business Portal, unaowawezesha kufanya malipo ya mkupuo kwa urahisi, ikiwemo kuwalipa wafanyakazi, wasambazaji au wadau wengine wa biashara kwa wakati mmoja.


“Kwa mfanyabiashara mwenye watu wengi anaotakiwa kuwalipa, mfumo huu unarahisisha kufanya malipo ya mkupuo badala ya kufanya miamala mmoja baada ya mwingine,” alisema.


Alisema timu ya mauzo ya kampuni hiyo ipo katika banda la YAS kuwapa wananchi maelezo ya kina, kuwaonesha namna ya kutumia mifumo hiyo na kuwasaidia kujiunga na huduma zinazowafaa kulingana na mahitaji yao.


Mbali na huduma za biashara, wananchi watakaotembelea banda hilo watapata fursa ya kujifunza matumizi ya Mixx Super App, inayowawezesha kuscan, kulipa bili, kununua bando na kufanya miamala mingine kwa urahisi.


Kampuni hiyo pia inaendesha kampeni yenye kaulimbiu, “Kila Muamala ni Bao la Ushindi,” inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali katika shughuli za kila siku.



🚨Full VIDEO Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post