TAMASHA LA 17 LA MUZIKI WA CIGOGO LAANZA RASMI DODOMA


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Tamasha la Kumi na Saba (17) la Muziki wa Cigogo limeanza rasmi leo Julai 24, 2026 katika viwanja vya Chamwino Arts Center (CAC), Chamwino-Ikulu, mkoani Dodoma, likiwa limekusanya wadau wa sanaa, utamaduni na vikundi vya muziki wa asili kutoka maeneo mbalimbali nchini.


Tamasha hilo, litakaloendelea hadi Julai 26, 2026, linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Kigogo pamoja na urithi wa sanaa za jadi za Tanzania kupitia maonesho ya muziki, ngoma za asili, semina na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.


Kwa mujibu wa ratiba ya siku ya kwanza, washiriki wataanza kwa kuwasili katika Chamwino Arts Center kwa ajili ya ziara ya utalii, kabla ya kutembelea Nyumba ya Tembe na kuona uchoraji wa ukuta wa Mama Tembe, shughuli zitakazoongozwa na Mkurugenzi wa Innovative Development for Future Generation (IDFG), Victoria Mponda.


Aidha, tamasha hilo litakuwa na maonesho ya wajasiriamali yatakayosimamiwa na Mratibu wa Tamasha, Sospeter Mapana, yakilenga kuwapa fursa wafanyabiashara na wabunifu kuonesha bidhaa na huduma zao kwa washiriki na wageni wa tamasha.


Wasanii watapata pia semina maalumu kuhusu fursa za ruzuku kutoka Nafasi Art Space, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kukuza taaluma zao kupitia ufadhili wa miradi ya sanaa na ubunifu.


Ratiba ya siku ya kwanza itahitimishwa kwa kuwasili kwa makundi mbalimbali ya sanaa katika Chamwino Arts Center, yakijiandaa kwa maonesho makubwa ya muziki na ngoma za asili yatakayofanyika katika siku zinazofuata.


Waandaaji wa tamasha wamewahimiza wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tamasha hilo, ambalo mbali na burudani, linatoa fursa ya kujifunza utamaduni, kukuza biashara na kuimarisha sekta ya sanaa nchini.




Previous Post Next Post