Na Mwandishi Wetu, Kongwa.📍
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Mayeka S. Mayeka, amekutana na wamiliki wa vibanda pamoja na wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo ya Kituo cha Mabasi, Posta na Sokoni, kwa lengo la kujadili umiliki halali wa vibanda hivyo pamoja na utekelezaji wa mfumo mpya wa kodi.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Elimu Kongwa, Mhe. Mayeka alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5, mmiliki halali wa vibanda vilivyopo katika maeneo hayo ni Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, huku watu waliovijenga wakitambuliwa kama wapangaji.
Alifafanua kuwa kodi ya awali ya shilingi 5,000 kwa mwezi imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko ya hali ya uchumi na mahitaji ya utoaji wa huduma, hivyo kuanzia sasa wafanyabiashara watalipa shilingi 20,000 kwa mwezi kwa kila banda.
Kwa mujibu wa utaratibu huo mpya, asilimia 70 ya fedha hizo, sawa na shilingi 14,000, itaelekezwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ili kuongeza mapato ya ndani na kuboresha huduma za maendeleo, huku asilimia 30, sawa na shilingi 6,000, ikipelekwa kwa waliovijenga vibanda hivyo kama fidia ya gharama za ujenzi.
Mhe. Mayeka alisema kabla ya kuanza kwa mikataba mipya, Serikali itafanya tathmini ya kila kibanda ili kubaini thamani ya ujenzi wake, hatua itakayowezesha fidia kulipwa kwa haki kwa walioviendeleza.
"Tutafanya tathmini ya ujenzi wa kila kibanda kabla ya kuanza mkataba mpya utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili. Baada ya kukamilika kwa malipo ya fidia ya ujenzi, waliovijenga vibanda watabaki kuwa wapangaji na wataanza kulipa kodi ya shilingi 20,000 kwa mwezi moja kwa moja Halmashauri," alisema Mhe. Mayeka.
Kwa upande wao, wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo walikiri kuwa kwa muda mrefu kulikuwepo na sintofahamu kuhusu umiliki wa vibanda hivyo kutokana na ukosefu wa elimu kuhusu sheria za ardhi na umiliki wa maeneo ya biashara.
Wafanyabiashara hao walieleza kuwa baada ya kupatiwa ufafanuzi na Serikali wamekubaliana kusaini mikataba mipya ya upangaji na kulipa kodi mpya, wakisema hatua hiyo itachangia kuongeza mapato ya Halmashauri na kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Kongwa.






