Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendelea kuthibitisha ubora wa huduma zake baada ya kutwaa Tuzo ya Mshindi wa Pili wa Mtoa Huduma Bora katika kategoria ya Mamlaka za Udhibiti kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yaliyofungwa Julai 13, 2026, jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla iliyohudhuriwa na Mgeni Rasmi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel, alisema mafanikio hayo yametokana na dhamira ya mamlaka hiyo ya kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali katika ununuzi wa umma.
Alisema katika kipindi chote cha maonesho, PPRA ilitoa elimu kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST katika kushiriki zabuni za umma na kuhamasisha uelewa wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, jambo lililowavutia na kuwafikia maelfu ya wananchi na wadau.
"Tuzo hii ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na watumishi wetu kwa ari, ubunifu na kujituma, sambamba na mazingira rafiki tuliyoyaandaa katika mabanda yetu mawili. Tunawashukuru Watanzania kwa kuendelea kutuamini na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha usimamizi wa ununuzi wa umma," alisema Bi. Mollel.
Alibainisha kuwa ushindi huo unakuja wakati PPRA ikiendelea kupata heshima kimataifa, baada ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Bw. Dennis Simba, kupokea tuzo mjini Geneva, Uswisi, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, kufuatia Mfumo wa NeST kutambuliwa kuwa miongoni mwa mifumo 20 bora duniani katika sekta ya Serikali Mtandao (e-Government).
Katika kategoria hiyo ya Mamlaka za Udhibiti, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitangazwa mshindi wa kwanza, huku PPRA ikishika nafasi ya pili kutokana na ubora wa huduma na elimu iliyotoa kwa wananchi wakati wa maonesho hayo.
