BRELA YANG'ARA SABASABA, YATWAA TUZO YA TATU KWA KUWEZESHA BIASHARA

 


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeendelea kudhihirisha mchango wake katika kuboresha mazingira ya biashara nchini baada ya kushinda tuzo ya nafasi ya tatu katika kundi la taasisi zinazowezesha biashara kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).


Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo iliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam, mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.


Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Seka Kasera, alisema ushindi huo ni uthibitisho wa mafanikio ya maboresho yaliyofanywa na taasisi hiyo katika utoaji wa huduma kupitia mfumo wa BRELA Online System (BOS).


Alisema mfumo huo umeongeza ufanisi wa huduma, kurahisisha upatikanaji wa huduma za usajili wa biashara na leseni, pamoja na kujenga imani kwa wananchi na wadau wa sekta ya biashara.


Kasera alieleza kuwa ushiriki wa BRELA katika maonesho ya mwaka huu umeiwezesha taasisi hiyo kusikiliza maoni ya wananchi, kutambua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kupata mrejesho muhimu utakaosaidia kuboresha huduma zaidi.


Alibainisha kuwa katika kipindi chote cha maonesho, BRELA ilitoa huduma mbalimbali zikiwemo usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni pamoja na elimu kwa umma kuhusu huduma zake, huku zaidi ya wafanyabiashara 1,200 wakinufaika na huduma zilizotolewa papo kwa papo.


Katika ushindani wa taasisi zinazowezesha biashara, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilishika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika nafasi ya pili, huku BRELA ikimaliza katika nafasi ya tatu na kuendelea kuthibitisha nafasi yake kama mdau muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Previous Post Next Post