WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MAGEREZA WAIMARISHA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA MAGEREZANI


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuimarisha jitihada za kuhakikisha haki inapatikana kwa wafungwa na mahabusu nchini, baada ya kufanya majadiliano maalumu na Jeshi la Magereza kuhusu kuboresha huduma za msaada wa kisheria magerezani.


Majadiliano hayo yamefanyika Juni 3, 2026 katika eneo la Mtumba jijini Dodoma, yakihusisha viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Jeshi la Magereza, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu nchini.



Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. John Jingu amesema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata haki kwa mujibu wa sheria, wakiwemo watu waliopo magerezani.


Amesema wafungwa na mahabusu wanahitaji msaada wa kisheria ili waweze kufahamu haki zao pamoja na taratibu mbalimbali za kisheria zinazowahusu, jambo ambalo litasaidia kuimarisha utoaji wa haki nchini.


Dkt. Jingu ameeleza kuwa maeneo muhimu ya ushirikiano huo ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wanaotoa huduma za msaada wa kisheria magerezani kupitia mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.


Aidha amesema Serikali inalenga kuimarisha mifumo ya utoaji wa haki kwa kutumia mbinu za kisasa pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa makundi yote yanayohitaji huduma hiyo.


“Matumizi ya mifumo ya kidijitali yataongeza ufanisi katika utendaji wa kazi, kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kuboresha huduma za msaada wa kisheria ndani ya magereza,” amesema Dkt. Jingu.



Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katungu ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano mkubwa unaoendelea kutolewa kwa Jeshi la Magereza, hususan katika kuwajengea uwezo maafisa wa magereza kupitia mafunzo na programu mbalimbali za kitaalamu.


Amesema huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa kwa wafungwa na mahabusu zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kutambua haki zao pamoja na kuelewa taratibu za kisheria, hatua ambayo imeongeza ufanisi wa utoaji wa haki ndani ya magereza.


Kamishna Katungu pia amepongeza juhudi za Wizara hiyo kwa kutoa vifaa vya TEHAMA vilivyosaidia kuboresha mawasiliano na utekelezaji wa majukumu ya kila siku ndani ya Jeshi la Magereza.


Majadiliano hayo yanatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha sekta ya sheria na haki nchini, huku yakilenga kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi.



🚨Subscribe YOUTUBE CHANNEL Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post