Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuhamasisha matumizi yenye tija ya umeme kwa kufikia vikundi vya ujasiriamali vya VICOBA katika Kitongoji cha Remiti, Mkoa wa Kilimanjaro. Kupitia ziara hiyo, wanachama wa vikundi hivyo walipatiwa elimu kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na upatikanaji wa umeme majumbani na katika shughuli zao za uzalishaji mali, kwa lengo la kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Akizungumzia umuhimu wa umeme katika maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo, Afisa Maendeleoya Jamii wa REA, Bi. Jaina Msuya, alisema kuwa REA imetembelea vikundi vinne vya wanawake wa jamii ya Kimasai na kuwahamasisha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi. “Tumewashauri kutumia fursa ya umeme kuanzisha shughuli kama mashine za kusaga nafaka, kusindika maziwa na samli pamoja na kuendeleza mazao mengine yatokanayo na mifugo,” alisema Bi. Msuya.
Viongozi wa vikundi vya VICOBA vya Remiti akiwemo Agnes Simon, Upendo Emmanuel, Namayan Emmanuel na Magdalena Michael wameishukuru Serikali kupitia REA kwa kuwafikishia huduma ya umeme ambayo imefungua fursa mpya za maendeleo katika jamii yao. Aidha, wameiomba Serikali kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mikopo ili waweze kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji na kuchangamkia kikamilifu fursa zinazotokana na nishati hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa REA Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Kelvin Melchiad, amesema kuwa jumla ya vitongoji 2,071 vimefikiwa na huduma ya umeme kati ya vitongoji 2,258 vilivyopo mkoani humo sawa na asilimia 91.7.
Aliongeza kuwa miradi miwili inayolenga kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote vilivyopo mkoani humo ipo katika utekelezaji ambapo mradi wa kupeleka umeme vitongojini Awamu ya II A unaotekelezwa na mkandarasi M/s Ceylex Engineering(pvt) Ltd kwa gharama ya Shilingi billioni 18.478 umefikisha umeme kwenye vitongoji 135 na utanufaisha wateja 4,455 wakati mradi wa kupeleka umeme vitongojini Awamu ya IIB unalenga kupeleka umeme kwenye vitongoji 186 na unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 33.5 na mkandarasi Derm Group(T) Ltd mradi na wateja 6,536 watanufaika.






