Na Jasmine Shamwepu, Dodoma.📍
Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimeitaka Serikali kuongeza juhudi katika kupambana na ndoa za utotoni kwa kufanya marekebisho ya sheria zinazotajwa kuwa kikwazo kwa ustawi wa mtoto wa kike na maendeleo ya elimu nchini.
Mkurugenzi wa TAWLA, Tike Mwambipile, amesema wamekutana na wabunge mjini Dodoma kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wa mtoto wa kike, ikiwemo changamoto ya ndoa za utotoni ambayo imeendelea kuathiri ndoto na mustakabali wa watoto wengi wa kike.
Mwambipile amesema wabunge wana nafasi kubwa ya kuwasilisha sauti za wananchi bungeni na kusukuma mabadiliko ya sheria yatakayolinda haki za watoto.
Amesema ndoa za utotoni si tu ukiukwaji wa haki za mtoto, bali pia ni kikwazo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuwa huwanyima watoto wa kike fursa ya kuendelea na elimu na kutimiza ndoto zao.
“Mzazi unapomuozesha mtoto katika umri mdogo unakatisha ndoto zake. Tunahitaji kuona watoto wa kike wanapata nafasi ya kusoma, kujijenga na kufikia malengo yao ya maisha badala ya kuingizwa katika majukumu ya ndoa kabla ya wakati,” amesema.
Mwambipile amesema TAWLA itaendelea kushirikiana na wabunge, Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha mazingira salama yanapatikana kwa watoto wa kike ili waweze kufikia uwezo wao kamili.
Kwa upande wao, wabunge wamekubaliana na hoja zilizowasilishwa na TAWLA na kueleza kuwa baadhi ya sheria zilizopo zinahitaji kufanyiwa mapitio ili kuendana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na sera za maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Mbunge wa Kasulu Mjini na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wabunge Tanzania (TWPG), Joyce Ndalichako, amesema kuna ulazima wa kuendelea kupitia sheria zinazoweza kuathiri ustawi wa mtoto wa kike, ikiwemo sheria zinazohusiana na umri wa kuingia kwenye ndoa.
Amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya kusoma na kupata maarifa yatakayomwezesha kujitegemea baadaye.
“Mtoto wa miaka 14 anatakiwa kuwa shuleni, siyo kuolewa. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika elimu na sasa watoto wengi wanapata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kumaliza elimu ya msingi. Hivyo, ni muhimu sheria zetu ziendane na malengo hayo,” amesema.
Ameongeza kuwa maono ya taifa yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yanasisitiza ustawi wa wananchi wote, hivyo kuna haja ya kuhakikisha sheria, sera na mifumo mbalimbali vinakwenda sambamba na lengo la kulinda haki za msingi za watoto na kukuza usawa wa kijinsia.








