Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina taarifa zinazoashiria kuwepo kwa mikutano inayofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambayo inadaiwa kuhusisha mipango ya kuhamasisha maandamano yenye uwezekano wa kuvuruga hali ya amani na utulivu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alisema chama hicho kinaendelea kuhimiza Watanzania kudumisha mshikamano, utulivu na amani kwa maslahi ya taifa.
Kihongosi alisema CCM inaamini kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana katika mazingira ya misukosuko ya kisiasa, akisisitiza kuwa tofauti za kiitikadi na kisera zinapaswa kujadiliwa kwa njia za amani na kupitia majukwaa halali ya kisiasa.
Alisema chama hicho kinatoa tahadhari kwa wananchi kutoshawishika kushiriki katika matukio yanayoweza kusababisha machafuko au kuhatarisha usalama wa nchi, akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwepo kwa vikao vinavyohusisha maandalizi ya maandamano ambayo yanaweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Tunawasihi wananchi wasishiriki katika mambo ya aina hiyo,” alisema Kihongosi.
Aidha, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu wa kuendelea kulinda utulivu wa nchi na kuhakikisha usalama wa wananchi pamoja na mali zao wakati wote.
Kihongosi pia aliwahimiza vijana kuelekeza nguvu zao katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuleta taharuki au migogoro.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapoona viashiria vya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.
Akizungumzia athari za maandamano, alisema mara nyingi madhara yake huwakumba wananchi wa kawaida zaidi kuliko wale wanaoyapanga au kuyahamasisha.
“Siasa za maendeleo zinapaswa kujengwa katika hoja na sera. Migogoro haijawahi kuleta suluhisho la kudumu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kihongosi alisisitiza umuhimu wa kuondoa kauli na vitendo vinavyoweza kuchochea mgawanyiko wa kijamii kwa misingi ya dini, kabila au maeneo ya kijiografia.
Akitoa taarifa kuhusu ziara za CCM katika maeneo mbalimbali nchini, alisema chama hicho kimebaini mwitikio mkubwa wa wananchi, ambao wamekuwa wakieleza changamoto zao pamoja na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema ziara hizo zilizofanyika katika mikoa kadhaa na wilaya zaidi ya 40 zimetoa fursa kwa viongozi wa chama kukutana moja kwa moja na wananchi, kusikiliza kero zao na kupokea maoni kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Kwa mujibu wa Kihongosi, wananchi wengi wameeleza kuona mabadiliko kupitia miradi inayotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hususan katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.
Alisema pia ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya ndani limeendelea kuiwezesha serikali kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi.
Kuhusu nafasi ya CCM katika siasa za Tanzania, Kihongosi alisema chama hicho kinaendelea kuwa imara kutokana na mtandao wake mpana wa uongozi unaofika ngazi za chini kabisa, hali inayokiwezesha kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi kwa haraka.
Aidha, alikanusha hoja kwamba CCM ni chama cha wazee pekee, akieleza kuwa chama hicho kina wanachama kutoka makundi yote ya umri na kwamba mchango wa wazee katika kujenga taifa na kuimarisha chama unaendelea kuwa muhimu.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

