Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Maandalizi ya Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo yanaendelea kwa kasi huku Mkoa wa Dodoma ukijiandaa kupokea mamia ya wadau wa sanaa na utamaduni watakaoshiriki tukio hilo kubwa la kitamaduni litakalofanyika Julai 24 hadi 26, 2026 katika viwanja vya Chamwino Arts Center, Chamwino-Ikulu.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha wasanii na vikundi vya ngoma za asili kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuendeleza na kuhifadhi tamaduni za jamii ya Wagogo pamoja na kukuza muziki wa asili wa Tanzania.
Kwa mujibu wa waandaaji, maandalizi ya tamasha hilo yamefikia hatua nzuri ambapo mazingira ya maonesho, mapokezi ya wageni pamoja na ratiba za ushiriki wa vikundi mbalimbali vinaendelea kupangwa ili kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa mafanikio makubwa.
Aidha, tamasha hilo linatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mikoa mbalimbali, hali itakayochochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi kupitia biashara ndogo ndogo, huduma za usafiri pamoja na sekta ya malazi na chakula.
Mbali na burudani ya muziki na ngoma za jadi, tamasha hilo pia litatumika kama darasa la utamaduni kwa vijana kwa kuwapa nafasi ya kujifunza mila, desturi na historia ya jamii ya Wagogo kupitia maonesho mbalimbali ya sanaa za asili.
Baadhi ya wadau wa sanaa wameeleza kuwa Tamasha la Muziki wa Cigogo limeendelea kuwa sehemu muhimu ya kukuza utamaduni wa Mtanzania na kuhamasisha jamii kuthamini urithi wa muziki wa jadi unaobeba historia na utambulisho wa taifa.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.



