MAGANYA: MAADILI NA UZALENDO VITAJENGA TAIFA IMARA


 Na Jasmine Shamwepu, Dodoma.📍



JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesema kauli iliyotolewa na mbunge wa Tunguu Zanzibar  Simai Mohamed  Said kuhusu uwepo wa Yuda (msaliti) ndani ya serikali haiwezi kuvuruga utulivu wa chama chao bali kitaendelea kuwa imara zaidi ya hapo awali.



Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Fadhili Maganya, alisema hayo jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Wazazi yanayotarajiwa kufanyika Julai 4, 2026, jijini Mwanza.



Alisema, CCM haiwezi kuteteleka kwa kauli iliyotolewa na mbunge huyo hivi karibuni wakati akichangia moja ya mjadala ya bajeti akidai kuwa ndani ya serikali yupo msaliti anayemuhujumu Rais.



"Chama Cha Mapinduzi kina wanachama zaidi ya milioni 15, wapo makada na wengine, na kila mmoja ana malezi yake na tabia zake. Haiwezekani mtu mmoja akaibuka na kutoa kauli yake ambayo itaweza kuharibu utulivu wa chama kitaendelea kuwa salama zaidi ya hapo awali," alisema Maganya



Aidha, alisema kauli hiyo iliyotolewa na mbunge huyo ni mtazamo wake binafsi na si wa chama kwani chama kina wasemaji wake na viongozi wengine wenye mamlaka kikatiba, na si kila mtu kutoa kauli zake.



"Chama chetu kina utaratibu wake yupo msemaji wa chama ambaye ni Mwenyekiti wetu, Samia Suluhu Hassan, lakini pia yupo Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti na Katibu wa Itikadi na Uenezi. Kama kauli hiyo haijatoka kwa hao, basi si msimamo wa chama, ni wa kwake binafsi," alisema



Akizungumzia maadhimisho ya Wiki ya Wazazi, alisema kilele kitafanyika Julai 4, 2026 jijini Mwanza, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Malezi Bora na Uzalendo ni Msingi wa Taifa.”



Maganya, alisema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa malezi bora, maadili na uzalendo katika kujenga taifa imara.



Pia, alisema katika siku ya maadhimisho kutakuwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali zikiwemo malezi, utamaduni, afya na mazingira, huku jumuiya hiyo ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha malengo ya maadhimisho hayo yanafikiwa.



Hata hivyo, alisema kabla ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na kongamano la kitaifa litakalojadili masuala ya malezi, maadili na uzalendo kwa taifa.



Ambalo,litawakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili malezi katika jamii.


Previous Post Next Post