CHODAWU YAIOMBA SERIKALI KURIDHIA MKATABA WA KAZI ZA STAHA KWA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI




Na Wellu Mtaki, Dodoma.

Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani Tanzania (CHODAWU) kimeiomba Serikali kuridhia Mkataba Namba 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani pamoja na kuboresha mfumo wa sheria zinazosimamia sekta hiyo.

Ombi hilo limetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa CHODAWU, Said Wamba, wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya mradi wa utetezi wa haki za wafanyakazi wa ndani na waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu.

Wamba amesema wafanyakazi wa majumbani ni kundi maalum lenye mazingira tofauti na wafanyakazi wa sekta nyingine, hivyo kuna umuhimu wa kuwepo kwa sheria na kanuni zinazoendana na mahitaji yao ili kulinda maslahi yao na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake, mdau wa maendeleo kutoka Shirika la Watu Wanaojitolea la Italia amesema ushirikiano huo unaonyesha mshikamano na uwajibikaji katika kupambana na changamoto zinazowakabili wanawake na wasichana wanaoendelea kukumbwa na unyonyaji na unyanyasaji.

Amesema lengo la ushirikiano huo ni kuimarisha ujuzi, maendeleo na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi kwa wafanyakazi wa majumbani nchini Tanzania, sambamba na kukabiliana na biashara haramu ya binadamu katika sekta hiyo kupitia uandaaji wa sera na kanuni bora.

“Kwa pamoja, tunalenga kuimarisha ujuzi, maendeleo na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi kwa wafanyakazi wa majumbani nchini Tanzania, huku wakati huo huo tukishughulikia changamoto ya biashara haramu ya binadamu katika sekta ya ajira za majumbani kwa kuandaa sera na kanuni stahiki,” amesema.



Aidha, amesisitiza kuwa Italia inaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda haki za wafanyakazi kupata ajira zenye staha pamoja na kuhimiza usawa wa kijinsia, akieleza kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kuheshimu utu na haki za binadamu.

“Hakuna maendeleo endelevu yanayoweza kupatikana bila kuheshimu utu wa binadamu,” amesema.
Previous Post Next Post