TANZANIA YADHIBITI TANI MILIONI 1.6 ZA VISUMBUFU VYA MIMEA, YAIMARISHA USALAMA WA CHAKULA.


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Serikali imesema imefanikiwa kudhibiti zaidi ya tani milioni 1.6 za visumbufu vya mimea ikiwemo nzige, ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea pamoja na panya katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2023 hadi 2025, hatua iliyochangia kuimarisha usalama wa chakula nchini na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.


Mafanikio hayo yameelezwa wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Afya ya Mimea Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda afya ya mimea ili kuondoa njaa, kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya uchumi.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema shughuli za kibinadamu zisizozingatia uwiano wa mazingira zimechangia kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuhatarisha afya ya mimea na usalama wa chakula duniani.


Amesema mimea ni msingi wa maisha ya binadamu kwani ndiyo chanzo kikuu cha chakula, dawa, malisho ya mifugo na huduma mbalimbali za mazingira ikiwemo kusaidia upatikanaji wa mvua na hewa safi.


“Kuongezeka kwa biashara za kimataifa pamoja na maendeleo ya sekta ya uchukuzi kumeongeza kasi ya usafirishaji wa mimea na mazao kutoka eneo moja kwenda jingine, hali inayorahisisha kusambaa kwa visumbufu na magonjwa ya mimea,” amesema Silinde.


Ameongeza kuwa ongezeko la watu duniani linaifanya dunia kuwa kwenye uhitaji mkubwa wa chakula, akitolea mfano takwimu za Umoja wa Mataifa zinazoonesha kuwa idadi ya watu duniani imefikia bilioni 8.2 mwaka 2025 na inatarajiwa kufikia bilioni 8.6 mwaka 2030 pamoja na bilioni 9 mwaka 2050.


Kwa mujibu wa Silinde, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula barani Afrika kupitia uimarishaji wa mifumo ya afya ya mimea na udhibiti wa visumbufu vya mazao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Plant Health and Pesticides Authority, Joseph Ndunguru amesema Tanzania imefikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130 katika mwaka 2024/2025 huku uzalishaji wa chakula ukifikia tani 23,783,128.


Prof. Ndunguru amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni mbalimbali za kudhibiti visumbufu vya mazao zilizotekelezwa nchini kote.


Amesema katika operesheni ya kudhibiti baa la panya iliyofanyika katika mikoa 19, zaidi ya ekari 408,109 za mazao ziliokolewa huku wakulima zaidi ya 66,511 wakinufaika moja kwa moja.


Aidha, amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti zaidi ya ndege waharibifu milioni 231 aina ya kwelea kwelea waliokuwa wakiharibu mashamba ya mpunga, mtama na uwele, hatua iliyookoa takribani tani 1,611,000 za mazao.


Katika kukabiliana na mashambulizi ya viwavijeshi, amesema TPHPA ilifanya operesheni za udhibiti katika hekta 219,411 kwenye wilaya 49 nchini na kufanikiwa kuokoa zaidi ya tani 529,347 za mazao ya mahindi na mtama.


Naye mwakilishi wa Food and Agriculture Organization nchini, Mushobozi Baitani amesema mabadiliko ya tabianchi pamoja na ongezeko la usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine vinaongeza kasi ya kuenea kwa magonjwa na visumbufu vya mimea kuvuka mipaka ya mataifa mbalimbali.


Amesema mdudu au kirusi mmoja anaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao, kupunguza kipato cha wakulima na kudhoofisha mifumo ya usalama wa chakula nchini.


Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mimea Duniani yamefanyika kwa mara ya nne kitaifa nchini Tanzania, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema: “Ulinzi wa Bayoanuai ya Mimea kwa Usalama wa Chakula na Lishe.”



🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA
Previous Post Next Post