MAANDALIZI TAMASHA LA 17 LA MUZIKI WA CIGOGO YAPAMBA MOTO DODOMA.



Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Maandalizi ya Tamasha la Kumi na Saba (17) la Muziki wa Cigogo yanazidi kushika kasi huku wadau wa sanaa, utamaduni na wakazi wa Mkoa wa Dodoma wakijiandaa kushuhudia burudani kubwa ya muziki wa asili itakayofanyika kuanzia Julai 24 hadi 26, 2026 katika viwanja vya Chamwino Arts Center, Chamwino-Ikulu, jijini Dodoma.


Tamasha hilo linalotarajiwa kukutanisha vikundi mbalimbali vya ngoma na muziki wa asili kutoka maeneo tofauti nchini, limeelezwa kuwa jukwaa muhimu la kuenzi na kuendeleza tamaduni za Kigogo pamoja na urithi wa sanaa za jadi za Tanzania.


Waandaaji wa tamasha hilo wamesema maandalizi yanaendelea vizuri ambapo tayari mipango ya ushiriki wa wasanii, maandalizi ya maeneo ya maonesho pamoja na huduma kwa wageni imekamilika kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha tamasha linafanyika kwa mafanikio makubwa.


Aidha, tamasha hilo linatarajiwa kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma, jambo litakalosaidia kukuza utalii wa ndani pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia biashara mbalimbali zitakazofanyika wakati wa tamasha hilo.



Mbali na burudani, tamasha hilo pia litatoa nafasi kwa vijana kujifunza historia, mila na desturi za jamii ya Wagogo kupitia nyimbo, ngoma na maonyesho ya utamaduni yatakayowasilishwa na vikundi vya sanaa.


Wadau wa sanaa wameeleza kuwa Tamasha la Muziki wa Cigogo limeendelea kuwa moja ya matukio muhimu ya kitamaduni nchini kutokana na mchango wake katika kulinda na kuhamasisha matumizi ya muziki wa asili kama sehemu ya utambulisho wa taifa.






🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA
Previous Post Next Post