MIRADI 54 YA MAENDELEO KUNG’ARA KWENYE MBIO ZA MWENGE DODOMA.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


MKOA wa Dodoma unatarajiwa kuanza rasmi mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 Mei 31, huku miradi 54 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 23 ikitarajiwa kupitiwa na Mwenge huo katika halmashauri zote za mkoa huo.


Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2026 jijini Dodoma na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mbio hizo muhimu za kitaifa.


Dkt. Kazungu amesema Mwenge wa Uhuru utapokelewa rasmi katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtera wilayani Mpwapwa kabla ya kuanza mbio zake katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.


Amesema katika kipindi chote cha mbio hizo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya zote saba pamoja na halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma kwa umbali wa kilomita 1,595.3.


Kwa mujibu wa Dkt. Kazungu, kati ya miradi 54 itakayopitiwa na Mwenge huo, miradi 21 itawekewa mawe ya msingi, miradi miwili itafunguliwa rasmi, miradi 20 itazinduliwa huku miradi 11 ikikaguliwa.


“Miradi yote inayotarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru ina thamani ya shilingi 23,243,056,418.58 na fedha hizo zimetokana na Serikali Kuu, mapato ya ndani ya halmashauri, michango ya wananchi pamoja na wafadhili na wadau mbalimbali wa maendeleo,” amesema Dkt. Kazungu.


Amefafanua kuwa Serikali Kuu imechangia zaidi ya shilingi bilioni 10.6, mapato ya ndani ya halmashauri zaidi ya shilingi bilioni 4.1, wananchi wakichangia zaidi ya shilingi bilioni 1.8 huku wafadhili na wadau wakitoa zaidi ya shilingi bilioni 6.6.


Aidha, amesema ratiba ya mbio hizo itaanza Mei 31 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kabla ya kuendelea katika Jiji la Dodoma Juni Mosi, kisha wilaya za Bahi, Kondoa, Kondoa Mji, Chemba, Chamwino na kumalizikia Kongwa Juni 7 mwaka huu.


Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 ni; “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”


Uongozi wa Mkoa wa Dodoma umehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na shughuli mbalimbali za Mwenge wa Uhuru kwa lengo la kuendeleza uzalendo, mshikamano na maendeleo ya Taifa.


Dkt. Kazungu amesema Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa alama muhimu ya matumaini, umoja na maendeleo kwa Watanzania wote.


🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu YA WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post