Na Carlos Claudio, Dodoma📍
WAZIRI MKUU, Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo kwa mamlaka, taasisi na wadau wote wanaosimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi na utawala wa sheria.
Akizungumza leo Jumatano, Aprili 8, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre wakati wa uzinduzi wa sera hiyo kwa niaba ya Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema changamoto zinazoikumba sekta ya ununuzi wa umma hazitokani na sera au sheria zilizopo, bali ni uzembe na mitazamo ya baadhi ya watendaji.
Amesema taarifa za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma zinaonesha wazi kuwa kasoro nyingi zinasababishwa na utekelezaji dhaifu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Sehemu kubwa ya changamoto hizi zinatokana na hulka, tabia na mitazamo ya watendaji. Hivyo, ni lazima tubadilike ili kufikia malengo ya sera hii,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu ameitaka sekta binafsi kujipanga vyema kwa kuimarisha ushirikiano na sekta ya umma ili kunufaika na fursa zilizopo ndani ya sera hiyo mpya.
Amesema sera hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kipato kwa wananchi pamoja na kujenga uchumi jumuishi na shindani.
Pia imeweka mwongozo mmoja unaounganisha hatua zote za mnyororo wa ugavi kuanzia ununuzi, uhifadhi, usambazaji hadi uondoshaji wa mali za umma.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, sera hiyo pia inalenga kuimarisha matumizi ya rasilimali za ndani, kukuza viwanda vya ndani, kuendeleza teknolojia pamoja na kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katika hatua nyingine, amezitaka wizara, taasisi na mamlaka zote kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazokinzana na sera hiyo ili kuweka mazingira rafiki ya utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema sera hiyo ni mwongozo muhimu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya ugavi katika sekta ya umma, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kudhibiti vitendo vya rushwa.
Amesema utekelezaji wa sera hiyo utaongeza ajira, kuimarisha mnyororo wa thamani na kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi kuelekea dira ya maendeleo ya mwaka 2050.
“Suala la mnyororo wa ugavi ni moyo wa uwajibikaji wa fedha za umma. Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa katika ununuzi na ugavi serikalini,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation Disability Hope (FDH), Maiko Salali, ameipongeza serikali kwa kuandaa sera jumuishi inayozingatia makundi maalum ikiwemo watu wenye ulemavu.
Amesema sheria ya ununuzi wa umma inayotenga asilimia 30 kwa makundi maalum imeendelea kuwapa fursa kubwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uchumi.
“Tumeridhishwa na namna sera hii ilivyozingatia ujumuishwaji. Hata watu wenye ulemavu wa kuona wamewezeshwa kuipata sera hii kupitia maandishi ya nukta nundu,” alisema.
Ameongeza kuwa uongozi wa Samia Suluhu Hassan umeleta mageuzi makubwa katika kuhakikisha kila kundi la kijamii linapata nafasi sawa katika maendeleo ya taifa.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na wadau wa sekta binafsi, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA







