SERA YA TAIFA YA UGAVI YAFUNGUA MILANGO KWA MAKUNDI MAALUM - MKURUGENZI MTENDAJI WA FDH

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation Disability Hope (FDH), Maiko Salali, ameipongeza serikali kwa kuandaa sera jumuishi inayozingatia makundi maalum, ikiwemo watu wenye ulemavu, hatua aliyoieleza kuwa ni muhimu katika kukuza usawa wa kijamii na kiuchumi nchini.


Akizungumza leo Jumatano, Aprili 8, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, Salali alisema sera hiyo imezingatia kwa kiasi kikubwa dhana ya ujumuishwaji.


Alieleza kuwa utekelezaji wa sheria ya ununuzi wa umma inayotenga asilimia 30 kwa makundi maalum umeendelea kufungua milango ya fursa kwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.


“Tumeridhishwa na namna sera hii ilivyozingatia ujumuishwaji. Hata watu wenye ulemavu wa kuona wamewezeshwa kuipata sera hii kupitia maandishi ya nukta nundu,” alisema Salali.


Aidha, alibainisha kuwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta mageuzi makubwa katika kuhakikisha kila kundi la kijamii linapata nafasi sawa ya kushiriki katika maendeleo ya taifa.



Uzinduzi huo ulifanyika chini ya mgeni rasmi, Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo alisisitiza umuhimu wa taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa sera hiyo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uwajibikaji.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na wadau wa sekta binafsi. 


Tukio hilo linaelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.




🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.


Previous Post Next Post