📌MITUNGI INA RUZUKU YA ASILIMIA 50 MAJIKO
Wananchi wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wamejitokeza kwa wingi kununua mitungi ya gesi ya kupikia inayotolewa kwa ruzuku ya asilimia 50 na Serikali, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi wengi kumudu gharama na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Usambazaji wa mitungi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hasa maeneo ya vijijini, ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Wananchi hao wameeleza kuwa mpango huo wa ruzuku, unaotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), utarahisisha maisha yao kwa kupunguza gharama za matumizi ya nishati na kuboresha shughuli za kila siku.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa usambazaji ulioanza Aprili 3, 2026 katika wilaya hiyo, wananchi walisema upatikanaji wa mitungi ya gesi utawasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kuchangia utunzaji wa mazingira pamoja na kurahisisha shughuli za mapishi.
“Hii ni nafuu kubwa kwetu. Sasa tunaweza kutumia gesi badala ya kuni na mkaa, jambo litakalotusaidia kuokoa muda na kulinda mazingira,” alisema mmoja wa wananchi.
Aidha, wananchi hao walimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa ruzuku hiyo, wakisema ni hatua muhimu katika kuboresha maisha ya Watanzania wa kipato cha chini.
Akizungumzia mradi huo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka REA, Bi. Jaina Msuya, alisema Wilaya ya Kisarawe imeanza kupokea mitungi ya gesi 3,255 yenye thamani ya shilingi 56,962,500, ambayo inauzwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500 kwa kila mtungi.
“Serikali imelenga kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, hivyo imeweka ruzuku ili kupunguza bei hadi kufikia shilingi 17,500,” alisema Bi. Msuya.
Aliongeza kuwa usambazaji wa mitungi hiyo umeanza kwa kuhusisha makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wakiwemo waendesha bodaboda, mama lishe pamoja na wafanyabiashara wa masokoni, ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Bi. Msuya, mnyororo wa thamani wa usambazaji wa gesi unatoa fursa nyingi za kiuchumi, ikiwemo biashara ya uwakala wa mitungi na vifaa vyake.
Aliwahimiza wanufaika kutunza mitungi hiyo vizuri na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kidogo kidogo ili waweze kumudu gharama za kujaza gesi pindi inapoisha.
Mradi huo wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia unatekelezwa katika wilaya zote za Tanzania Bara kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuboresha ustawi wa wananchi.








