SERIKALI YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA KUIMARISHA HUDUMA ZA KIDIGITALI ZANZIBAR.

 


Na Carlos Claudio, Zanzibar📍


Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu imekabidhi vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo kompyuta 36, kwa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidigitali (DTP).


Makabidhiano hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora (Sheria House), yakilenga kuimarisha utendaji kazi serikalini pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia za kidigitali.



Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Fatma Mabrouk Hamis, alisema kuwa vifaa hivyo vitachangia kuongeza ufanisi kwa watumishi wa umma, sambamba na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika taasisi za serikali.


Alieleza kuwa matumizi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku yakirahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Alisisitiza kuwa vifaa hivyo vitaongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kusaidia utoaji wa huduma kwa haraka, usalama na uwazi.


Aidha, alibainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza ajenda ya uchumi wa kidigitali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa ufanisi na kwa wakati.



Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidigitali (DTP), Bakari Mwamgugu, alisema lengo kuu la mradi huo ni kuhuisha na kuimarisha mifumo ya serikali ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi.


Alifafanua kuwa “kusomana kwa mifumo” ni uwezo wa mifumo mbalimbali ya kielektroniki kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa usalama, hatua inayosaidia kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.


Mwamgugu aliongeza kuwa mradi huo pia umewezesha utoaji wa vifurushi vya intaneti vyenye ukubwa wa Gigabaiti 20 (GB 20) ili kurahisisha matumizi ya mtandao, huku mfumo wa kubadilishana taarifa unaojulikana kama Zan e-Exchange chini ya Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar (e-GAZ) ukitarajiwa kukamilika hivi karibuni.


Alisema vituo vya pamoja vya utoaji huduma vimeanzishwa ili kuwasaidia wananchi kupata huduma mbalimbali za serikali katika eneo moja, hususan kwa wale wanaopata changamoto ya kufika katika ofisi za serikali, kwa kuwa sasa wanaweza kupata huduma za kidigitali wakiwa walipo.


Kwa mujibu wa Mwamgugu, taasisi 211 tayari zimeunganishwa na mkongo wa taifa, zikiwemo hospitali, shule na taasisi mbalimbali za serikali, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utoaji wa huduma kwa njia za kidigitali.


Aidha, watendaji 450 wa serikali wamepatiwa mafunzo katika teknolojia zinazoibukia kama vile Akili Unde (AI), Internet of Things (IoT), Ujifunzaji wa Mashine (Machine Learning) na Usalama wa Mtandao (Cyber Security).


Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mansoura Mosi Kassim, alisema vifaa hivyo vitaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo.


Alishukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa ni kielelezo cha kuimarika kwa Muungano, huku akiahidi kuwa vifaa hivyo vitatumika ipasavyo kufanikisha azma ya kujenga Zanzibar ya kidigitali.


Mradi wa Tanzania ya Kidigitali ulianza mwaka 2021 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2026, ukiwa umechangia kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza teknolojia na uchumi wa kidigitali.




🚨Full Video Inapatikana katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post