Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema anaunga mkono rasmi ombi la Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kupandishwa hadhi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda na kuwa Hospitali ya Taifa, akieleza kuwa taasisi hiyo tayari ina sifa za kutoa huduma za kiwango cha juu kitaifa na kimataifa.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bodi ya pili ya Wadhamini ya BMH, Mhe. Mchengerwa alisisitiza kuwa atalitetea ombi hilo kwa Samia Suluhu Hassan kila atakapopata fursa ya kuonana naye ili kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Alisema BMH ni “kioo cha Dodoma na Taifa kwa ujumla,” akibainisha kuwa hospitali hiyo imekuwa mfano wa utoaji wa huduma bora za afya, ikiwa na mazingira safi, uongozi thabiti na watumishi wenye dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi.
“Katika sekta ya afya nimekuwa nikisikia malalamiko mengi kutoka maeneo mbalimbali, lakini sijawahi kusikia malalamiko yanayoihusu BMH. Hii ni ishara kuwa mnafanya kazi nzuri sana,” alisema Mchengerwa huku akiwapongeza viongozi na watumishi wa hospitali hiyo.
Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa hatua ya kuipandisha hadhi BMH itaambatana na maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi, kuimarisha vifaa tiba, kuboresha miundombinu pamoja na kuanzisha huduma mpya za kisasa. Alisisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha huduma zote za kibingwa bobezi zinapatikana Dodoma, kama ilivyokuwa dhamira ya Julius Nyerere wakati wa kuhamishia makao makuu ya nchi hiyo mjini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa aliipongeza Bodi mpya ya Wadhamini wa BMH akisema wajumbe wake ni wataalamu wenye uzoefu mkubwa katika sekta ya afya, na kuwataka kuhakikisha wanasimamia kikamilifu maendeleo ya hospitali hiyo kwa kukamilisha miradi inayoendelea, kuanzisha mipya na kuifanya kuwa kitovu cha utalii tiba nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Edward Hoseah, alimuomba Waziri kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili hospitali hiyo, ikiwemo upungufu wa watumishi, uhaba wa magari ya huduma na madeni yanayofikia shilingi bilioni 14.39 kutoka taasisi na wadau mbalimbali waliopatiwa huduma.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Abel Makubi, alisema katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, kumekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za afya, huku akibainisha kuwa hatua ya kuipandisha hadhi itakuwa chachu ya kuimarisha zaidi ubora wa huduma na kuongeza imani kwa wananchi.
Hatua ya kuipandisha hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha huduma za kibingwa na maendeleo ya sekta ya afya nchini.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.





