MAWASILIANO SAHIHI NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUFANIKISHA HUDUMA ZA CHANJO.

 


Ubora na ufanisi wa huduma za chanjo unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa mawasiliano sahihi, yanayowezesha jamii kupata taarifa za kuaminika na kwa wakati kuhusu umuhimu wa chanjo.


Hayo yamesemwa  Jijini Arusha na Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya wakati wa Mafunzo kwa Viongozi Wasimamizi wa Huduma za Chanjo (Mid-level Managers Training in Immunization Services - MLM) yanayohusisha washiriki kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.


Nzilibili amesema mawasiliano bora ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha jamii inaelewa umuhimu wa chanjo, hivyo kusaidia kuongeza mwitikio wa wananchi kujitokeza kupata huduma hiyo muhimu ya kinga.


Ameeleza kuwa utoaji wa elimu sahihi kwa jamii unasaidia kuondoa dhana potofu, uvumi na upotoshaji unaoweza kusababisha baadhi ya watu kusita au kukataa chanjo. “Ni muhimu kuhakikisha taarifa zinazotolewa kwa umma ni sahihi, wazi na zinawafikia walengwa kwa wakati ili kujenga uelewa na imani kwa jamii,” amesema.


Aidha, amesisitiza kuwa watumishi wa afya wanapaswa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo mikutano ya jamii, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe sahihi wa chanjo kwa wananchi.


Ameongeza kuwa kushirikiana na viongozi wa jamii, dini na makundi mbalimbali ni hatua muhimu katika kuimarisha uelewa wa wananchi na kupunguza upotoshaji wa taarifa kuhusu chanjo.


Katika kuimarisha huduma za chanjo, Nzilibili amebainisha kuwa mawasiliano madhubuti huchangia kuongeza uelewa wa ratiba za chanjo, umuhimu wake pamoja na madhara ya kukosa chanjo, hivyo kusaidia kupunguza magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.


Kwa kuhitimisha, ametoa wito kwa wadau wote wa afya kuendelea kuwekeza katika mawasiliano ya afya kwa umma, akisisitiza kuwa elimu sahihi na endelevu kwa jamii ni msingi wa mafanikio ya programu za chanjo na ulinzi wa afya ya wananchi.







🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA
Previous Post Next Post